King Combs aamini babake huenda akaachiliwa mapema

Marion Bosire
1 Min Read
Diddy na mwanawe King Combs

King Combs mwana wa kiume wa mwanamuziki anayezuiliwa Sean Diddy Combs anaamini kwamba babake huenda akaachiliwa kabla ya kukamilika kwa kifungo chake.

Alikuwa akisafiri kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Los Angeles almaarufu Lax alipokabiliwa na wanahabari.

Kijana huyo wa umri wa miaka 27 ambaye pia ni mwanamuziki wa mtindo wa rap aliambia wanahabari hao kwamba kama familia watakuwa wakicheza wimbo wa “Diddy Free” likizo hii wakishikilia matumaini kwamba hilo huenda likatimia.

Alifichua kwamba babake anaendelea vyema gerezani Fort Dix huko New Jersey na kwamba naye pia ana imani kwamba ataachiliwa mapema.

Diddy alikamatwa kwa mara ya kwanza Septemba 2024 kwa mashtaka kadhaa kama uhalifu wa mtandao, usafirishaji wa watu kwenda kutumika kingono na kusafirisha watu kushiriki katika ukahaba.

Kesi yake ilisikilizwa na kuamuliwa mwaka huu wa 2025 na baraza la waamuzi ambalo lilimwachia huru kwa makosa makubwa zaidi lakini alipatikana na hatia kwa makosa mawili ya “kusafirisha watu kushiriki katika ukahaba” chini ya sheria za Marekani.

Mwezi Oktoba 2025, alihukumiwa kifungo cha miezi 50 gerezani.

Anatakiwa pia kulipa faini ya dola laki 5 na atakuwa chini ya uangalizi kwa miaka mitano baada ya kumaliza kifungo.

Share This Article