Makala ya nane ya patashika ya kombe la CHAN yatarejea leo kwa mechi za semi fainali nchini Uganda na Tanzania.
Mamba wa Sudan watakuwa na miadi dhidi ya Madagascar kuanzia saa kumi na moja unusu katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Sudan wanajivunia kutopoteza mechi wakimaliza nafasi ya kwanza kundini D kwa alama 5, wakishinda mechi moja na kutoka sare mbili.
Katika Robo fainali Sudan wanaonolewa na Kwesi Apiah, waliwatema nje Algeria kwa mabao 4-2 kupitia mikiki ya penati kufuatia sare ya 1-1.
Upande waoMadagascar walishinda mechi mbili na kupiga sare moja na kushindwa moja wakimalia nafasi ya pili kundini B.

Katika robo fainali waliilemea Kenya mabao 3-2, kupitia penati baada ya sare ya 1-1 katika dakika 120.
Nusu fainali ya pili itawakutanisha miamba Morocco, ambao wametawazwa mabingwa mara mbili, dhidi ya mabingwa watetezi Senegal kuanzia saa mbili unusu usiku.
Morocco walimaliza wa pili kundini A wakishinda mechi tatu na kupoteza moja na kisha kuwabandua wenyeji wenza Tanzania goli moja bila.
Senegal walichukua pia nafasi ya pili kundini D kwa pointi 5 wakishinda moja na kwenda sare 2.
Katika robo fainali waliwatema nje Uganda kwa goli moja bila jawabu.