Serikali inafuatilia kwa makini hatua zinazopigwa katika utekelezaji wa miradi yake, kuhakikisha mfumo wa kuimarisha uchumi kutoka chini almarufu BETA, unafanikiwa.
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, alisema serikali imetoa kipaumbele katika sekta za kilimo, uvuvi, uchimbaji madini na uchumi wa baharini, kuongeza mapato ya wananchi walio katika viwango vya mashinani.
Kuhusu kampeni ya kitaifa ya kuwachanja mifugo iliyoanzishwa leo katika kaunti ya Laikipia, naibu huyo wa Rais alisema shughuli hiyo itawaletea wafugaji mapato ya kumezewa mate.
Kulingana na Kindiki, hatua hiyo ndio sababu kuu ya kuanzishwa kwa shughuli ya kuwachanja mifugo.
Alisema licha ya Kenya kuashikilia nafasi ya tatu kati ya mataifa yenye mifugo wengi barani Afrika, haiwezi kuuza nje bidhaa za mifugo kutokana na athari ya magonjwa.
Prof. Kindiki aliyasema hayo Alhamisi, aliposhiriki meza ya mazungumzo na viongozi kutoka kaunti ya Isiolo waliomtembelea afisini mwake mtaani Karen.