Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, amesema serikali inajitahidi kutekeleza miradi ya maendeleo katika sehemu zote za nchi, huku akiwashutumu wale wanaojaribu kugawanya taifa hili kwa misingi ya kikabila.
Akizungumza Ijumaa wakati wa mkutano wa uwezeshaji kaunti ya Machakos, Naibu huyo wa Rais alihakikisha kuwa hakuna taifa ambalo litatengwa katika utawala wa Kenya Kwanza.
“Kila kaunti, kila wadi, zitanufaika na miradi ya maendeleo ambayo itaimarisha maisha ya wananchi,” alisema Kindiki.
Alidokeza kuwa serikali kuu kwa sasa inajenga masoko 15 ya kisasa, nyumba za bei nafuu, zikiwemo nyumba za wanafunzi wa chuo kikuu na wale wa vyuo vya kiufundi, miongoni mwa miradi mingine.
Aidha aslisema usambazaji umeme kwa makazi umepanuliwa, serikali ikilenga kuunganisha nyumba 6,500 kwa umeme kwa kitita cha shilingi bilioni nne.
Wakati huo huo, Naibu huyo wa Rais alisema serikali iko makini kuhakikisha jamii zote hapa nchini zinaishi kwa amani, ili kuchochea maendeleo.