Kindiki awashutumu wanasiasa wanaofanya kampeni za mapema

Huku ikiwa imesalia miaka 2 kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, wanasiasa wa mirengo yote wameanza kampeni za kujinadi kwa Wakenya, ishara kwamba uchaguzi huo utakuwa moto wa kuotea mbali.

Martin Mwanje
1 Min Read
Kithure Kindiki - Naibu Rais

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amewaonya baadhi ya wanasiasa wanaojihusisha na kampeni za mapema akisisitiza kuwa huu ni wakati wa kuwahudumia Wakenya wala sio kufanya siasa za pesa nane. 

Amesema wakati wakiwa madarakani, wanasiasa hao hawakufanya chochote cha kuwanufaisha Wakenya, na kwa misingi hiyo wanapaswa kufyata mdomo hadi wakati mwafaka wa kampeni uwadie.

Aliyasema hayo wakati akiwahutubia viongozi wa mashinani 1,500 kutoka kaunti ya Isiolo.

Na ili kudhihirisha kuwa serikali ya Kenya Kwanza imo mbioni kuwahudumia Wakenya, Naibu Rais alisema serikali inatoa kipaumbele kwa ukamilishaji wa barabara yenye urefu wa kilomita 750 inayoanzia Mandera hadi Isiolo.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo utakamilishwa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana naye, ujenzi wa barabara zenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,000 unaendelea kaskazini mwa nchi, hatua aliyoitaja kuwa ya kwanza chini ya utawala wa Rais William Ruto.

 

 

 

Share This Article