Kindiki akagua ujenzi wa kituo cha ufugaji samaki na utoaji mafunzo cha Kabonyo

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki akagua ujenzi wa kituo cha ufugaji samaki na utoaji mafunzo cha Kabonyo.

Naibu Rais Prof. Kithure kindiki, amekagua ujenzi unaoendelea wa kituo cha ufugaji samaki na kutoa mafunzo cha Kabonyo, eneo la Nyando kaunti ya Kisumu.

Wakati wa ziara hiyo, Kindiki alitoa wito kwa wanakandarasi wanaotekeleza mradi huo, kuuharakisha ili uweze kuwafaidi wakazi wa Kisumu.

Mradi huo utakaogharimu shilingi bilioni 1.3, ni mojawepo wa miradi ya serikali ya taifa inayolenga kumarisha uchumi wa baharini na sekta ya ufugaji samaki hapa nchini.

Kituo hicho ambacho ujenzi wake uko katika asilimia 15, utakapo kamilika utatoa mbegu milioni 28 za samaki kila mwaka kufanikisha ufugaji samaki katika ziwa Victoria.

“Utakapo kamilika mwezi Juni mwaka 2026, kituo hiki kitatoa mbegu za samaki na kusambaza kwa wakulima wadogo wadogo na wale wanaotekeleza kilimo cha samaki kwa kiwango kikubwa,” alisema Kindiki.

Mradi huo unanuia kuwawezesha mamilioni ya wakenya katika ufugaji wa samaki pamoja na kuimarisha shughuli za uchumi katika kaunti zilizo karibu na ziwa Victoria za Migori, Homabay, Kisumu, Siaya na Busia.

Share This Article