Kimbunga cha Fung-wong kimepita kwenye Bahari ya Kusini ya China na kinatarajiwa kuelekea Taiwan, baada ya kusababisha vifo vya watu wawili nchini Ufilipino.
Takriban watu milioni 1.4 nchini Ufilipino walikuwa wamehamishwa kabla ya kimbunga Fung-wong kutua Jumapili kikibeba upepo wa kasi ya 185km/h (115mph) na dhoruba za 230km/h (143mph).
Kimekumba eneo la Aurora huko Luzon – kisiwa chenye watu wengi zaidi nchini – saa 21:10 saa za eneo (13:10 GMT) na kudhoofika saa chache baadaye.
Kimbunga Fung-wong kinajiri siku chache baada ya kimbunga cha Kalmaegi kilichosababisha vifo vya takriban watu 200.
Mamlaka ya Ufilipino inaripoti uharibifu mdogo kuliko ilivyotarajiwa – ingawa jamii kadhaa bado zimetatizika kutokana na mafuriko.
Kulipopambazuka, upepo wa Kimbunga Fung-wong zilizokuwa zimevuma usiku kucha zilikuwa zimeisha, na watu wakatoka kuona uharibifu.
Kulikuwa na uharibifu mkubwa wa majengo, lakini maandalizi mazuri yanaonekana kuzuia kurudiwa kwa athari zilizoonekana baada ya kimbunga Kalmaegi kukumba eneo la kati la Ufilipino wiki iliyopita.