Kijana akamatwa kwa kukosea heshima bendera ya Kenya

Marion Bosire
2 Min Read

Polisi wamekamata kijana wa umri wa miaka 17 aliyenaswa kwenye video iliyosambaa mitandaoni akiikosea heshima bendera ya Kenya wakati wa mechi ya kandanda katika Uwanja wa Nyayo.

Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Idara ya Upelelezi wa Jinai – DCI ilithibitisha kuwa Ibrahim Haidar Yusuf, mmoja wa wanaosakwa kuhusiana na tukio hilo, amekamatwa.

Tukio hilo lilitokea Septemba 20, 2025, wakati wa mechi kati ya Mogadishu City Club na Police FC.

Video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha vijana wawili wakikanyaga, kuipiga teke na kuidhalilisha bendera ya taifa, jambo lililozua hasira na shutuma kutoka kwa umma, mitandaoni na uwanjani.

“Kitendo hiki ni kinyume cha sheria na kinavunjia heshima maadili na thamani tunazoziheshimu kama taifa. Juhudi za kumkamata mshukiwa wa pili, ambaye inaaminika yuko nchini, zinaendelea,” DCI ilisema.

Kulingana na Kifungu cha 2B cha Sheria ya Bendera ya Kitaifa, Alama na Majina, Sura ya 99, yeyote anayeonesha dharau kwa bendera ya taifa, wimbo wa taifa au alama zilizobainishwa anatenda kosa la jinai.

Waziri wa usalama wa taifa Kipchumba Murkomen aliagiza kukamatwa, kufunguliwa mashtaka na kufukuzwa nchini kwa wahusika iwapo ni wageni, akilielezea tukio hilo kuwa la kusikitisha na lisilokubalika.

Balozi wa Somalia nchini Kenya, Jabril Ibrahim Abdulle, naye alilaani vikali tukio hilo, akikanusha kuwa nchi yake inahusiana kwa namna yoyote na vitendo vya mashabiki wa Mogadishu City FC.

Share This Article