Mamlaka ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi (IPOA) sasa inasema imeanzisha uchunguzi kuhusiana na kifo cha Simon Warui aliyefariki akiwa kwenye seli katika kituo cha polisi cha Central jijini Mombasa.
Kwa mujibu wa Chama cha Wanasheria nchini, LSK, Warui aliripotiwa kutoweka juzi Jumapili asubuhi (Septemba 21), majira ya saa nne asubuhi na ripoti za kifo chake kuzuka siku hiyo.
Hata hivyo, kulingana na IPOA, Warui alifariki Jumatano wiki iliyopita, Septemba 17.
“Hii ni kuelezea kuwa IPOA imeanza kukusanya ushahidi; kuhoji mashuhuda na kupitia upya taratibu za maafisa wa polisi kuhusiana na kisa hicho,” alisema mwenyekiti wa IPOA Issack Hassan kwenye taarifa.
“Isitoshe, imepata ripoti ya upasuaji inayobaini sababu ya kifo kuwa ‘kilichotokana na kushindwa kupumua kutokana na kuteguka kwa shingo kunakoendana na kuanguka kutoka juu.”
Issack amesisitiza umuhimu wa watu waliozuiliwa kwenye seli kuhakikishiwa usalama wao na kuahidi kufanya kila awezalo kuhakikisha haki inatendeka.
“Tunauhakikishia umma kuwa IPOA itashughulikia suala hili kwa dhati na kutuma risala za rambirambi kwa familia ya marehemu,” aliongeza mwenyekiti huyo wa IPOA.
Taarifa yake ikikuja siku moja baada ya Chama cha Wanasheria nchini, LSK kumteua wakili wa kuiwakilisha familia huku uchunguzi ukiendelea kubaini namna kifo cha Simon Warui kilivyotokea wakati akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Mombasa.
“LSK inafuatilia kisa cha Bw. Simon Warui aliyefariki wakati akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Central, Mombasa. Tumemteua wakili wa kuiwakilisha familia katika kufuatilia uchunguzi unaoendelea na kuhakikisha ukweli kamili na hali iliyosababisha kifo cha Bw. Warui vinawekwa wazi, na mtu aliyehuika kuwajibishwa,” alisema Rais wa LSK Faith Odhiambo kwenye taarifa hiyo jana.
“Tumepokea ripoti kutoka kwa familia zinazoashiria kwamba alitoweka majira ya saa nne asubuhi siku ya Jumapili na ripoti kupigwa katika kituo cha polisi cha Embakasi. Hali iliyosababisha kifo chake katika kituo cha polisi cha Mombasa bado haijulikani, lakini tunafanya kazi kwa karibu na washirika wa mashirika ya kijamii na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu KNCHR kuhakikisha suala hilo linachunguzwa haraka na kuhitimishwa.”
Kifo cha Warui kinatokea takriban miezi miezi minne baada ya kile cha Albert Ojwang kutokea katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi.
Hadi kufikia sasa, IPOA ambayo imekuwa ikifanya uchunguzi wa kubaini waliomuua Ojwang haijatoa ripoti ya matokeo ya uchunguzi wake.