Kifo cha Mohbad: washukiwa waondolewa lawama

Watatu hao pamoja na wengine walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika kifo cha Mohbad.

Marion Bosire
2 Min Read
Marehemu Mohbad, mwanamuziki wa Nigeria

Mahakama nchini Nigeria imeondolea lawama washukiwa watatu wa kifo cha kutatanisha cha mwanamuziki Ilerioluwa Oladimeji Aloba maarufu kama Mohbad.

Abdulazeez Fashola almaarufu Naira Marley, Samson Balogun Eletu maarufu kama Sam Larry na Owodunni Ibrahim maarufu kama Primeboy wameondolewa lawama kuhusiana na kifo cha msanii huyo.

Mohbad aliaga dunia Septemba 12, 2023 akiwa na umri wa miaka 27 na wengi walinyosha vidole vya lawama kwa Naira Marley mmiliki wa kampuni iliyokuwa imemsajili Mohbad ya Marlian Records, Sam Larry na Primeboy.

Kulingana na ushauri wa kisheria kutoka kwa kurugenzi ya mashtaka ya umma, hakimu Ejiro Kubenje alitoa uamuzi kwamba watatu hao hawana kesi ya kujibu.

Mahakama ilisema pia kwamba washukiwa wengine wawili ambao ni muuguzi aliyehudumia Mohbad kabla ya kifo chake na mmoja wa marafiki wa Mohbad.

Muuguzi huyo aitwaye Feyisayo Ogedengbe na rafiki ya Mohbad aitwaye Ayobami Sadiq, wana kesi ya kujibu kutokana na utepetevu wao kinyume na sehemu ya 251 (e) ya sheria dhidi ya uhalifu.

Naira Marley, Sam Larry na Prime boy walikamatwa na maafisa wa polisi kuhusiana na kifo cha Mohbad mwaka 2023 lakini wakaachiliwa kwa dhamana huku kesi ikiendelea.

Uvumi ulisambaa mitandaoni wakati huo kwamba watatu hao huenda walimpa sumu Mohbad ikasababisha kifo chake lakini uchunguzi wa maiti yake ukabaini kwamba alifariki kutokana na madhara ya mchanganyiko wa dawa alizokuwa amepatiwa.

Share This Article