Gavana wa zamani wa kaunti yaNairobi, Evans Kidero, sasa yuko huru baada ya mahakama kuu jijini Nairobi kumwondolea mashtaka ya ufisadi katika kesi iliyohusu shilingi milioni 213.
Hii ni baada ya mahakama kuamua kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka yote 17 ya ufisadi yaliyomhusisha yeye na washitakiwa wengine tisa, huku jaji akisema hakukuwa na ushahidi tosha kuthibitisha tuhuma hizo.
Jaji Victor Wakumile alibainisha kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha bila shaka kwamba washtakiwa walifanya malipo kwa kampuni mbili kwa ajili ya bidhaa na huduma ambazo hazikuwahi kutolewa.
Licha ya kumwondolea Kidero mashtaka, mahakama ilisema aliyekuwa mkuu wa idara ya uhasibu katika kaunti ya Nairobi bado ana kesi ya kujibu, baada ya jaji kueleza kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha kuhitaji majibu kutoka kwake.
Kidero, ambaye alikuwa Gavana wa kwanza wa Nairobi mwaka 2013 hadi 2017, alikuwa ameshtakiwa kwa makosa ya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi, ikiwemo njama ya kutenda kosa la ufisadi, matumizi mabaya ya mamlaka, na upatikanaji wa mali ya umma kwa njia ya udanganyifu.
Alisomewa mashtaka hayo pamoja na maafisa wengine wa zamani wa Kaunti ya Nairobi, wakiwemo katibu wa kaunti, afisa mkuu wa fedha, waziri wa fedha na mipango, kaimu afisa mkuu wa fedha, na kaimu mkuu wa hazina.
Watu hao walidaiwa kushirikiana kutekeleza udanganyifu uliosababisha kupotea kwa shilingi milioni 213 za serikali ya kaunti kati ya Januari 16, 2014 na Januari 25, 2016.