Huduma ya taifa ya misitu KFS imetangaza kwamba iko macho kutokana na visa kadhaa vya moto kwenye isitu nchini, huku ikionya kwamba misitu iko katika hatari kubwa kufuatia hali ya sasa ya hewa.
Huku visa vya hivi maajuzi katika misitu ya Mau, Mlima Kenya na Aberdare vikiwa vimethibitiwa kikamilifu, KFS inasisitiza umakini katika vituo vyake vyote kote nchini.
Hatua hii inafuatia hali inayojiri ya kiwango cha juu cha joto, kiwango cha chini cha unyevu na upepo mkali ambayo inaweka misitu katika hatari ya moto.
Kulingana na KFS, tangu Januari 2025, visa vya moto vimeongezeka nchini hasa katika maeneo kama vile Isiolo, Garissa, na Pwani.
Katika muda wa wiki moja iliyopita visa 180 vya moto vimenakiliwa ambavyo vimeharibu ekari 1,357.97 za misitu katika hifadhi mbali mbali kama Maasai Mau, North Rift na katika nyanda za juu za katikati mwa nchi.
Kutokana na hayo, KFS imesimamisha uchomaji wa aina yoyote wa mimea karibu na misitu na imeweka masharti makali ambapo kila mmoja lazima apate idhini iliyoandikwa ya kuchoma mimea kabla ya kufanya hivyo.
Huduma hiyo ya misitu imeimarisha pia utayari wake wa kukabiliana na visa vya moto kwa kugawa vifaa zaidi vya kuzima moto katika vituo vyake na kurejesha kazimi wafanyakazi wote ili kuhakikisha uwepo wa nguvukazi.
Shirika hilo la kutunza misitu limeweka pia mfumo wa kutambua moshi katika maeneo ya misitu kwa ufuatiliaji wa wakati.
Linashirikiana pia na jamii zinazoishi karibu na misitu, mashirika mengine ya serikali na washirika wa utunzaji mazingira ili kukomesha visa vya moto na uharibifu zaidi.