KESSHA yaonya shule zinaweza kufungwa mapema kufuatia ukosefu wa fedha

Tom Mathinji
2 Min Read
KESSHA yailaumu serikali kwa kuchelewesha fedha za kugharamia masomo.

Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari nchini (KESSHA) kimeonya kuhusu uwezekano wa shule kufungwa mapema iwapo pesa za kugharimia masomo hazitatolewa haraka.

KESSHA imesema ukosefu wa fedha hizo umevuruga shughuli za kila siku na kuathiri ubora wa elimu kote nchini.

Akizungumza na wanahabari katika kaunti ya Murangá, Katibu Mkuu wa chama hicho Abdinoor Haji alisema ucheleweshwaji wa kutolewa kwa fedha hizo umesababisha viwango vya elimu kudorora, na ndio chanzo kikuu cha upatikanaji wa alama za E katika mitihani ya kitaifa ya KCSE kwa muda wa miaka mitatu iliyopita.

“Shule za kutwa ndizo zimeathiriwa zaidi kwa sababu zinategemea pakubwa fedha hizo za serikali. Ukosefu wa fedha hizo umedumaza uwezo wa kufanikisha upatikanaji wa elimu bora,” alilalama Haji.

Aidha, kulingana na Katibu huyo Mkuu, kutokana na ukosefu wa fedha, shule nyingi zimeshindwa kuwalipa wasambazaji bidhaa huku baadhi ya shule zikilazimishwa kuwaachisha kazi walimu walioajiriwa na Bodi za Usimamizi wa shule.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa KESSHA Willy Kuria alilalamika kwamba shule za sekondari zinaidai serikali shillingi bilioni 17 za muhula  wa kwanza na wa pili.

Alionya kuwa iwapo Wizara ya Elimu itakosa kulipa malimbikizi hayo ya madeni, shule zitalazimika kufungwa mapema kwa sababu ya ukosefu wa pesa za kuwaweka wanafunzi shuleni.

TAGGED:
Share This Article