Kesi ya Lissu yaahirishwa kwa mara nyingine

Wakili mkuu wa serikali aliambia mahakama kwamba mkurugenzi wa mashtaka ya umma bado anadurusu faili ya kesi hiyo.

Marion Bosire
2 Min Read
Tundu Lissu, Kiongozi CHADEMA

Kesi ya uhaini inayomkabili mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu imeahirishwa kwa mara nyingine, hadi Julai 15, 2025.

Hakimu mkuu mkazi wa mahakama ya Kisutu Franko Kiswaga alitaja sababu za kuahirishwa kwa kesi hiyo kuwa hatua ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma yaani DPP kuomba hilo.

Kulingana na Kiswaga, mashtaka yanayomkabili Lissu yamevutia umma kwa kiwango kikubwa na yana uzito ndiposa muda zaidi unahitajika  kudurusu faili ya kesi.

Tundu Lissu ambaye alifikishwa mahakamani leo Julai Mosi, 2025, alipinga hatua ya kuahirisha kesi hiyo mara kadhaa akisema kwamba mahakamani sio mahali pazuri pa kukaa.

Alihimiza upande wa serikali pia ujitokeze na kutangaza kwamba hautaki tena kuendelea na kesi hiyo kutokana na kile anachodai kuwa ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria, anapendekeza pia kwamba kesi hiyo ihamishiwe mahakama kuu akishangaa muda anaochukua DPP kudurusu faili.

Wakili mkuu wa Serikali Nassoro Katuga alisema kuwa shauri hilo lina maslahi kwa umma ndio maana wameomba liahirishwe ili waje kusema hatua ambayo imefikiwa katika kudurusu hati za kesi hiyo.

Kuhusu CHADEMA kuzuiwa kushiriki uchaguzi mkuu ujao, Lissu alisema mahakamani kwamba msajili wa vyama vya kisiasa hana mamlaka ya kuzuia chama chochote kushiriki shughuli za siasa katika mwaka wa uchaguzi.

Lissu anadaiwa kutenda kosa hilo la uhaini Aprili 3, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, pale aliposhawishi umma kuzuia maandalizi ya uchaguzi mkuu.

Share This Article