Kesi ya Diddy kuanza leo

Mchakato wa kusikiliza kesi dhidi ya mwanamuziki huyo unaanza leo kwa hatua ya uteuzi wa kundi la waamuzi.

Marion Bosire
2 Min Read
P Diddy

Kesi dhidi ya mwanamuziki Sean “Diddy” Combs inaanza leo Jumatatu Mei 5, 2025 huko New York, na hatua ya kwanza ni kuteua kundi la waamuzi.

Watu wengi ulimwenguni wanafuatilia kwa makini kesi hii kwa sababu kwa wakati fulani, Diddy alikuwa na ushawishi wa kiwango cha juu na hakuna ambaye angeamini kwamba siku moja atafika alipo sasa.

Combs wa umri wa miaka 55 sasa analaumiwa kwa makosa ya ulanguzi wa binadamu kwa ajili ya kuwatumia kingono na amesubiri kesi dhidi yake tangu mwaka jana.

Anadaiwa kuongoza uhalifu ambao waendesha mashtaka wanautaja kuwa kulazimisha wahanga wake kuhusika kwenye sherehe za ngono zilizokuwa zikiendeshwa na pombe na mihadarati.

Mwanamuziki huyo anaripotiwa kutishia wahanga wake na hata kushambulia wengine iwapo wangekataa alichokuwa akitaka au kujaribu kufichua matendo yake.

Tayari Combs amekanusha mashtaka yote dhidi yake akisisitiza kwamba matendo yoyote ya kingono yalifanyika baada ya makubaliano kati ya wahusika na hivyo hakuna aliyelazimishwa

Katika kikao cha hivi maajuzi cha maandalizi ya kesi hiyo, wakili wa Diddy Marc Agnifilo aliangazia utetezi wa kundi lakehuku akitaja mtindo wa maisha wa Diddy kuwa wa mtu anayependa kufanya ngono na watu tofauti.

Diddy alijikusanyia mali nyingi kutoka kwa kazi yake ya muziki na biashara nyingine kama ya pombe katika muda wa miongo kadhaa.

Hatua ya kuteua kundi la waamuzi inatarajiwa kukamilika katika muda wa wiki moja huku taarifa za ufunguzi wa kesi hiyo zikitarajiwa kusomwa mahakamani Mei 12, 2025.

Combs amekuwa kizuizini tangu Septemba 2024 alipokamatwa na amenyimwa dhamana mara kadhaa.

Share This Article