Mahakama ya hakimu ya Milimani jijini Nairobi imefutilia mbali kesi iliyokuwa imewasilishwa na bintiye Rais Charlene Ruto dhidi ya mwandishi Webster Ochora baada ya Charlene kukosa kufika mahakamani.
Hakimu Robinson Ondieki katika uamuzialiotoa leo Novemba 24, 2025, alikubali ombi la mkurugenzi wa mashtaka ya umma – DPP la kuondoa kesi hiyo baada ya pande husika kuwasilisha makubaliano ya kusuluhisha jambo hilo mahakamani.
Ondieki alisema kwamba kifungu cha 176 cha Kanuni ya mwenendo wa mashauri ya Kiraia, kinachoruhusu mahakama kuhimiza upatanisho, uhamasisho na kuwezesha suluhu ya kesi, kilitumika katika uondoaji wa kesi hiyo.
Mahakama iliongeza kuwa kesi hiyo kati ya pande husika ni ya kibinafsi.
Mapema mwezi huu, Charlene Ruto aliomba mahakama iruhusu kesi dhidi ya Webster Ochora itupiliwe mbali bila yeye kuhitajika kufika mahakamani binafsi.
Kupitia wakili wake, Kevin Kachapin, Bi. Ruto alifahamisha mahakama kuwa alikuwa amemwandikia mkurugenzi wa mashtaka ya umma waraka, akiomba mteja wake akubaliwe kutofika mahakamani kutokana na ufuatiliaji mkali wa vyombo vya habari na uchunguzi wa umma kuhusu jambo hilo.
Hata hivyo, upande wa mashtaka uliiambia mahakama kuwa maagizo ya DPP yalikuwa kesi iondolewe chini ya Kifungu cha 204 cha Kanuni ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambacho kinamtaka mlalamishi kufika binafsi mahakamani ili kuiondoa rasmi.
Hakimu Robinson Ondieki alijibu akibainisha kuwa DPP ana mbinu za kuondoa kesi bila uwepo wa mlalamishi.
Charlene katika waraka wake alielezea kwamba kesi hiyo imefuatiliwa sana na vyombo vya habari na umma, na kwamba kutokuwepo kwake kutasaidia kuepusha vurugu za umma zisizo za lazima na kuhakikisha kuwa mchakato unalenga madhumuni yake ya kisheria.
Webster Ochora alikuwa ameshtakiwa kwa kujisingizia kuwa mtu mwingine chini ya Kifungu cha 382(1) cha Kanuni ya Adhabu.
Alijisingizia kuwa binti ya Rais Ruto, Charlene Ruto na kutumia jina la Zawadi Publishers kuandika na kusambaza kitabu kiitwacho “Beyond the Name: Charlene Ruto and the Youth Uprising”.