Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA nchini TanzaniaTundu Lissu, atasalia gerezani kwa muda kufuatia kuahirishwa kwa kesi inayomkabili ya uhaini kwa mara nyingine.
Hakimu anayesikiliza kesi hiyo katika mahakama ya hakimu mkazi ya Kisutu, alikubali ombi la mawakili wa Jamhuri ya Tanzania la kuahirisha kesi hiyo kwa mara nyingine hadi Julai 30, 2025.
Kabla ya uamuzi huo kutolewa, Lissu ambaye anajiwakilisha mwenyewe, ikitizamiwa kwamba kitaaluma yeye ni mwanasheria, aliomba mahakama isikubali ombi la mawakili wa serikali la kuahirisha kesi hiyo.
Alishangaa ni kwa nini faili ya kesi yake inacheleweshwa kwa muda mrefu na wahusika hawasemi imefikia wapi, huku akilalamikia kuendelea kukaa gerezani katika mazingira yasiyo mazuri.
“Badala ya kutuletea maneno, wanastahili kutwambia faili imeshakwenda mahakama kuu, ndivyo sheria inavyosema” alisema Lissu mahakamani alipopatiwa fursa ya kujitetea.
Kiongozi huyo wa upinzani aliendelea kulalamika kwamba amefungwa katika sehemu moja na wafungwa sugu waliohukumiwa kunyongwa na anataka kesi yake iwasilishwe katika mahakama kuu haraka iwezekanavyo.
Alikamatwa tarehe tisa mwezi Aprili mwaka huu, kutokana na kampeni ambayo alikuwa anaendesha ya kusema kwamba hakutakuwepo na uchaguzi iwapo mabadiliko hayangefanywa.
Aprili 10 2025, alifikishwa mahakamani Kisutu kwa mara ya kwanza ambapo alishtakiwa kwa uhaini kwa kuchochea wananchi kususia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuandaliwa mwezi Oktoba mwaka huu.