Huduma ya Taifa ya Ukaguzi wa Mimea (KEPHIS) imeanzisha mchakato wa kupinga marekebisho ya sheria ya mbegu na aina za mimea yaliyopendekezwa kwenye mswaada wa mabadiliko ya sheria hiyo wa mwaka 2025.
Kulingana na KEPHIS, iwapo marekebisho hayo yatapitishwa, huenda yakalemaza uwezo wa serikali wa usimamizi, kudunisha ubora wa mbegu na kusababisha hali ya kuchanganyikiwa miongoni mwa wakulima.
Mswada huo ulio katika Bunge la Seneti kwa sasa unapania kuanzisha mpango mbadala wa kusajili aina za mbegu kupitia kwa Shirika la Ubora wa Bidhaa (KEBS), hatua ambayo KEPHIS inasema itakuwa ni sawa na kugawa majukumu yaliyo sawa na kudunisha jukumu lake kisheria.
Akizungumza katika ofisi ya kamishna wa kaunti ya Uasin Gishu wakati wa mpango wa majadiliano na wadau, Mkurugenzi wa KEPHIS Theophilus Mutui alisema wakulima huenda wakajipata katika hali ya sintofahamu kuhusu ni asasi gani wanapaswa kushirikiana nayo kwa mbegu bora iwapo KEBS itakuwa mhusika.
Aidha, alisema itakuwa makosa kukubali watengenezaji mbegu kubaini ubora wa mbegu zao wenyewe na hivyo kudunisha majukumu ya KEPHIS.