Kenzo akanusha madai ya kuzuia wasanii kwenye kampeni za NRM

Marion Bosire
2 Min Read
Eddy Kenzo

Mwanamuziki wa Uganda Eddy Kenzo amekanusha madai kwamba amekuwa akizuia wasanii kupata fursa ya kutumbuiza kwenye mikutano ya kampeni ya chama tawala cha NRM.

Kenzo ambaye ni mshauri wa Rais Kaguta Museveni kuhusu masuala ya wasanii ameamua kuzungumzia uvumi unaoenezwa kuhusu kutoelewana kati yake na mwanamuziki mwenza Bebe Cool kuhusu utumbuizaji kwenye mikutano ya kampeni ya NRM.

Madai yaliyosambaa mitandaoni yanasema kwamba Kenzo amekuwa akizuia wanamuziki maarufu kitaifa nchini Uganda na wale kutoka eneo la kati mwa nchi hiyo huku akipendelea wasanii walio na ushawishi kimaeneo.

Wadadisi wanahisi kwamba Kenzo anakosesha wasanii wengine mapato ya mikutano hiyo ya kampeni ya chama tawala. Uamuzi wa Kenzo unaripotiwa kumkera Bebe Cool ambaye amejukumiwa kusimamia wasanii kwenye kampeni na kuwapa malipo.

Kenzo amejitokeza kujibu madai hayo akisema kwamba uamuzi wake ulikuwa wazi na ulilenga kuhakikisha usawa na wala zio kukuza ushindani.

Akizungumza katika mahojiano Kenzo aliuliza, “Hebu fikiria iwapo wasanii kutoka Buganda wangetumbuiza watano huku wale wa kutoka Kaskazini wakiwa kama 20, ingekuwa sawa kweli?”

“Nilichotaka ni kwamba wasanii wa maeneo husika wapate pia fursa ya kutumbuiza nyumbani” aliendelea kusema Kenzo.

Kampeni zimeshika moto nchini Uganda kwa sasa ambapo wananchi wanatarajiwa kuchagua viongozi wao kwa muhula mwingine Januari mwaka 2026.

Rais Museveni ndiye mwaniaji wa Urais wa chama chake cha NRM.

Share This Article