Kenzo adai umaarufu wa NUP unadidimia

Marion Bosire
2 Min Read
Eddy Kenzo

Mwanamuziki Eddy Kenzo, ambaye pia ni rais wa Shirikisho la Wanamuziki Uganda yaani Uganda National Musicians Federation – UNMF, amesema kwamba Chama cha National Unity Platform (NUP) kinapoteza umaarufu.

Kenzo ambaye pia ni mshauri wa Rais Yoweri Museveni kuhusu wabunifu alisema hilo linafanyika kwa kasi na chama cha NUP kinahitaji kujipanga upya endapo kinatarajia kurejesha mvuto wake wa kitaifa.

Akizungumza wakati wa mahojiano, Kenzo alidai kuwa mwelekeo wa sasa wa chama unaonyesha dalili za kudhoofika, akiongeza kuwa baadhi ya wafuasi wake wakuu mtandaoni wanafanya madhara kuliko manufaa.

“Ningependa kuwashukuru wanajeshi wote wa NUP kwa kazi kubwa wanayoifanya. Lakini wanapaswa kuwa waangalifu sana wanapomvamia mtu kama mimi, kwa sababu mimi ni mmoja wa waanzilishi. Matunda wanayofurahia, sisi ndio tulipanda.” Alisema.

Kenzo, ambaye katika miaka ya hivi karibuni amejitenga na NUP na sasa anaunga mkono waziwazi chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), alidai kuwa alishiriki juhudi za awali zilizoimarisha umaarufu na ushawishi wa NUP kabla ya kuwa chama kikuu cha upinzani.

Alipendekeza kuwa chama hicho kinachoongozwa na mwanamuziki Bobi Wine, kinapaswa kutafuta ushauri kutoka kwa waanzilishi kama yeye ili kurejesha kasi yake kwa sababu wanajua alichowafanyia na bado anaweza kufanya zaidi.

Kenzo anasisitiza kuwa wakosoaji wake wanapaswa kuheshimu mchango wake na kuelekeza nguvu katika kukijenga upya chama badala ya kuvunja wale waliokisaidia kupanda.

Share This Article