Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amewataka wanachama wa chama cha upinzani ODM kuendeleza urithi wa marehemu kiongozi wa chama hicho marehemu Raila Amolo Odinga.
Uhuru alituma ujumbe kwa wanachama wa chama hicho kupitia kwa katibu mkuu Edwin Sifuna, wanapoadhimisha miaka 20 ya uwepo wa chama hicho huko Mombasa.
Katika ujumbe wake Rais huyo wa zamani alimtaja Raila kuwa nguvu ya kipekee katika mapambano ya muda mrefu ya Kenya ya kuafikia haki na mabadiliko kisiasa.
Sifuna alisoma ujumbe huo wakati wa dhifa iliyoandaliwa jana kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya chama hicho, ikilenga waanzilishi wa chama.
Rais Mstaafu Uhuru alisema chama hicho ni lazima kisimame kwenye misingi ya maadili ambayo yanaashiria juhudi za Raila za miongo kadhaa za kutafuta nchi yenye usawa.
Kiongozi huyo alisema kwamba kutokuwepo kwa Raila kunaendelea kuhisiwa kote nchini huku akimtaja Raila kuwa zaidi ya kiongozi wa chama.
Uhuru alimtaja Raila kuwa moyo wa mapambano aliyoongoza kwa miaka kadhaa na dhihirisho la ujasiri, uvumilivu na imani isiyotikisika ya kuafikia ndoto ya Kenya.
Alimalizia kwa kusema kwamba Kujitolea kwa Raila pamoja na uongozi wake viliongoza mapambano ya haki na kuchora ramani ya mabadiliko ya kisiasa ya Kenya.
Chama cha ODM kinaandaa tamasha la siku tatu huko Mombasa kama njia ya kuadhimisha miaka 20 ya chama hicho. Tamasha hilo lilianza Ijumaa na litafikia kilele leo Jumapili.