Serikali ya Kenya imechukua hatua kubwa kuelekea kufanikisha Huduma ya Afya kwa Wote (UHC) kwa kuzindua rasmi TaifaCare na Ajenda ya Mageuzi ya Afya Kidijitali katika Kaunti ya Nyandarua.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Afya Aden Duale alieleza kuwa TaifaCare ni mwelekeo mpya na wa kipekee wa kugharamia huduma za afya kwa njia inayohakikisha Wakenya wote wananufaika.
Walengwa wanajumuisha walioajiriwa rasmi, wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi na watu walio katika mazingira magumu, ambao bima yao itagharamiwa kikamilifu na serikali.
“TaifaCare sio tu mpango mwingine wa bima ni mabadiliko ya msingi katika mfumo wetu wa afya,” alisema Waziri Duale.
“Kupitia zana za kidijitali, mama aliye Kipipiri au mgonjwa aliye Wajir ataweza kupata taarifa zake za matibabu kutoka sehemu yoyote nchini Kenya, akipata huduma kwa heshima na kwa wakati.” Aliongeza.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Dkt. Mercy Mwangangi, alisisitiza jukumu la SHA katika kuhakikisha usawa na uwajibikaji.
Alieleza kuhusu hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF), ile ya Huduma za Afya ya Msingi (PHCF) na ile ya Dharura, Magonjwa Sugu na Hali Mahututi (ECCIF) zote zikiwa na lengo la kulinda wananchi dhidi ya gharama kubwa za matibabu.
Ubunifu kama Lipa SHA Pole Pole na mchakato wa madai wa kidijitali umeletwa ili kuondoa vizingiti vya kifedha na kujenga upya imani ya wananchi kwa mfumo wa bima ya afya.
Mamlaka ya Afya Kidijitali (DHA) ilionyesha jinsi digitali inavyoboresha ufanisi na uwazi katika mfumo mzima wa afya.
Zana kama AfyaYangu, Practice360 na Rekodi za Afya za Kielektroniki (EHRs) zitaruhusu wagonjwa kupata huduma katika kaunti yoyote, huku mifumo kama Rejesta ya Wahudumu wa Afya Kidijitali na uchambuzi wa data kubwa (big data analytics) ikiongeza uwezo wa kupanga na kusimamia sekta ya afya.
Kaunti ya Nyandarua inaibuka kama kinara katika utekelezaji wa mpango huu, ikiwa tayari imetoa vifaa vya kidijitali kwa Wahamasishaji wa Afya Jamii 1,249 (CHPs), na zaidi ya vifaa 600 kusambazwa katika vituo vya afya vya umma 88 kama sehemu ya Mitandao ya Huduma ya Afya ya Msingi (PCNs) na mfumo mpya wa Usimamizi wa Taarifa za TaifaCare.
Gavana wa Kaunti ya Nyandarua, Mheshimiwa Dkt. Moses Kiarie Badilisha, alisifu juhudi za serikali kuu katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya mashinani.
Aliahidi kuwa serikali yake iko tayari kuhakikisha utekelezaji kamili wa TaifaCare katika kaunti hiyo, akisisitiza kuwa mageuzi ya kidijitali na mifumo imara ya kifedha ya afya yataboresha maisha na utu wa wakaazi wa Nyandarua.
“Hii ni siku ya fahari kwa Nyandarua. Tunasimama kidete kuiunga mkono ajenda hii ya mabadiliko ya afya, na tumejipanga kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma,” alisema Gavana Badilisha.
Wizara ya Afya, SHA, na DHA ziliwataka wadau wote — wakiwemo serikali za kaunti, watoa huduma binafsi, wabunifu wa teknolojia, na washirika wa maendeleo — kuunga mkono mageuzi haya makubwa.
Waziri Duale alihitimisha kwa kusema: “Hili ni mbegu ya ufanisi, usawa, na ubora — huduma ya afya kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.”
Timu kutoka Wizara ya Afya na taasisi zingine za serikali itatembelea Nyandarua kukamilisha mchakato wa kuipandisha hadhi Hospitali ya J.M. Kariuki kuwa Hospitali ya Rufaa ya Ngazi ya 5.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi katika Kaunti ya Nyandarua leo mchana, Waziri wa Afya Mheshimiwa Aden Duale alimhakikishia Gavana Badilisha kwamba, pamoja na kuipandisha hadhi hospitali hiyo, itapewa hadhi ya kuwa kituo cha mafunzo ya madaktari wanaofanya mafunzo kwa vitendo (internship), hivyo kusaidia kuwapa nafasi madaktari wapya nchini.
Viongozi hao wawili walikuwa wakihutubia mamia ya wataalamu wa afya waliohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi katika viwanja vya Hospitali ya J.M. Kariuki, iliyolenga kuongeza uelewa kuhusu huduma za bima ya TaifaCare na kuhamasisha wahudumu wa afya ya msingi kuhusu mpango huo mpya.