Kenya imezindua rasmi taasisi yake ya kitaifa ya afya ya umma – KNPHI hatua muhimu inayolenga kupiga jeki uwezo wa taifa hili katika kugundua, kushughulikia na kuzuia dharura za afya nchini.
Hafla ya uzinduzi katika jumba la KICC iliadhimisha kile ambacho viongozi husika walikitaja kuwa mwamko mpya katika usalama wa afya kitaifa.
Waziri wa Afya Aden Duale, ambaye aliongoza hafla hiyo alisisitiza kwamba uzinduzi wa taasisi hiyo ni sehemu ya kujitolea kwa serikali kwa ajenda ya kuwezesha watu kiuchumi kuanzia chini almaarufu Bottom-Up Economic Transformation Agenda – BETA.
Ajenda hiyo kulingana naye inatoa kipaumbele kwa kuhakikisha ustahimilivu wa mpango wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wote – UHC.
“Utayari, ugunduzi wa mapema na ushughulikiaji wa haraka sio hiari ni hatua muhimu.” alisema waziri Duale akiongeza kusema kwamba taasisi ya afya ya umma inatoa jukwaa la pamoja la kutoa kipaumbele kwa afya ya umma, kuondoa kurudiwa kwa majukumu na kuhakikisha hatua za haraka zilizoratibiwa wakati wa majanga.
Taasisi ya KNPHI, iliasisiwa kisheria kupitia arifa ya serikali Januari 2022 na inaunganisha idara 13 kuu za Afya na mipango ambazo ni pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa, oparesheni za dharura na maabara za kitaifa za afya ya umma.
Uunganishaji huu ni mabadiliko muhimu ya kimfumo katika utawala wa afya wa Kenya unaolenga kuwianisha juhudi za serikali na viwango vya kimataifa kama vile kanuni za afya za shirika la afya ulimwenguni WHO.
Mwakilishi wa WHO nchini Daktari Abdourahmane Diallo naye alisisitiza kuhusu umuhimu wa kujenga taasisi zenye uwezo akisema, “Uthabiti wa uwezo wa taifa wa kusimamia vitisho vya kiafya ni sambamba na mifumo na watu wanaohusika.”
Diallo alisifia Kenya akisema “Leo imepanda mti wenye nguvu. Kazi inaanza sasa.”
Hafla ya uzinduzi wa KNPHI ulihudhuriwa na maafisa wakuu serikalini, wataalamu wa Afya na washirika wa kimaendeleo.
Waziri Duale alihimiza tume ya utumishi wa umma iharakishe uidhinishaji wa nguvu kazi ili kuhakikisha taasisi hiyo inaafikia uwezo kamili wa kutekeleza shughuli zake.