Kenya yawasilisha mpango wa pili wa Kitaifa wa tabianchi kwa UNFCCC

Kenya ilitimiza tarehe ya mwisho ya mawasilisho iliyowekwa na UNFCCC ya Aprili 30, 2025 na kuthibitisha tena kujitolea kwake kwa hatua za kimataifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Marion Bosire
2 Min Read
Waziri wa Mazingira Debora Barasa.

Serikali ya Kenya imewasilisha rasmi mchango wake wa pili wa kitaifa iliodhamiriwa kwa mkataba wa umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (UNFCCC).

Haya ni kulingana na tangazo lililotumwa na waziri wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi na misitu Deborah Baraza kwa vyombo vya habari.

Katika wasilisho hilo, Kenya imeelezea ramani ya njia ya hatua zake za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kipindi cha mwaka 2031 hadi 2035.

Kwa kutimiza tarehe ya mwisho ya mawasilisho iliyowekwa na UNFCCC ya 30 Aprili 2025, Kenya imethibitisha tena kujitolea kwake kwa hatua za kimataifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kupitia mkakati jasiri na jumuishi.

Mchango huu mpya uliotayarishwa kwa kushirikisha wadau, umeweka malengo makubwa ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi kwa asilimia 35 kufikia mwaka 2035.

Ili kutimiza lengo hili, Kenya inapanga kufadhili asilimia 20 ya juhudi hizo kwa rasilimali za ndani na kutafuta msaada wa kimataifa kwa asilimia 80 iliyosalia ikijumuisha fedha za tabianchi, uhamishaji wa teknolojia na ushiriki katika masoko ya kaboni.

Gharama yote ya utekelezaji inakadiriwa kufikia dola bilioni 56 za Marekani, ambapo takriban dola bilioni 10.5 zinatarajiwa kutokana na vyanzo vya ndani.

Uwasilishaji huu unaangazia maono ya Kenya ya kujenga jamii iliyo thabiti dhidi ya tabianchi na unaweka kipaumbele katika hatua za mabadiliko, upotevu na uharibifu, pamoja na maendeleo endelevu ya muda mrefu.

Mchango wa Kenya unatarajiwa pia kuchochea ubunifu na ukuaji jumuishi wa kiuchumi, huku marekebisho yajayo yakilenga kulingana na ajenda ya maendeleo ya Kenya baada ya mwaka 2030.

Waziri wa Mazingira, mabadiliko ya tabianchi na misitu Deborah Barasa, ameitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono mpango huu wa kimapinduzi wa Kenya, akisisitiza nafasi ya nchi hii kama kiongozi katika juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Share This Article