Kenya yawasiliana na Tanzania kuhusu usalama wa raia wake

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri mwenye Mamlaka Makuu aliye pia waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi.

Waziri mwenye Mamlaka Makuu aliye pia waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi, ameshauriana na mwenzake wa Tanzania balozi Mahmoud Thabit Kombo kushughulikia usalama wa raia wa Kenya wanaofanyakazi na kuishi nchini Tanzania kufuatia ghasia za Uchaguzi Mkuu zilizoghubika taifa hilo.

Kwenye mazungumzo hayo, Mudavadi alisisitiza umuhimu wa kulinda haki, usalama, na heshima ya jamii ya Kenya, ambayo inaendelea kuleta athari chanya katika uchumi wa Tanzania kupitia ujasiriamali, biashara, na huduma za kitaaluma.

Mudavadi alisema walijadili ripoti za hivi karibuni zinazohusisha matukio ambapo haki za baadhi ya raia wa Kenya zilikiukwa.

“Kuhusiana na haya, ripoti rasmi zimewasilishwa kwa mamlaka ya Tanzania ili  hatua madhubuti kuchukuliwa. Mimi na Kombo tumekubaliana kwamba wasiwasi wowote unaojitokeza utashughulikiwa kupitia njia za kidiplomasia na kibalozi zilizoanzishwa, kwa kufuata kikamilifu mikataba ya kimataifa na kanuni za Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Mudavadi.

Walielezea kujitolea kwao kuimarisha uhusiano wa kihistoria wa nchi hizo mbili, uliokitwa kwenye mizizi ya heshima, ushirikiano na utangamano wa kikanda.

Share This Article