Kenya yawapongeza makamishna wapya wa AUC

Tom Mathinji
1 Min Read
Kenya yawapongeza Makamishna wapya wa AUC

Serikali ya Kenya imekubali matokeo ya uchaguzi wa Makamishna wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), ulioandaliwa wakati wa mkutano wa 38 wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Kupitia kwa taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ilimpongeza Mahmoud Ali Youssouf, ambaye alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa AUC na Balozi Selma Malika Hadadi aliyechaguliwa kuwa Naibu mwenyekiti, pamoja na Makamishna wapya waliochaguliwa.

Taarifa hiyo ilielezea imani ya Kenya kwa uongozi huo mpya wa AUC, ikisisitiza kuwa kupitia uongozi wao, Umoja wa Afrika (AU) utakuwa katika fursa nzuri kuafikia malengo yake kuambatana na ajenda ya mwaka 2063.

“Tuna imani kwamba chini ya uongozi huu mpya, Umoja wa Afrika utaimarika kuliwezesha bara hili kuafikia ajenda ya mwaka 2063,” ilisema taarifa hiyo.

Serikali pia ilichukua fursa hiyo kupongeza kampeni ya mwaniaji wa Kenya kwenye wadhifa wa mwenyekiti wa AUC Raila Odinga, ikisema kampeni hiyo ilileta matumaini kwa wengi barani humu, na aliwakilisha Kenya kwa heshima, taadhima na bidii wakati wa mchakato huo.

Kenya pia ilizishukuru nchi za Afrika zilizomuunga mkono Raila, ikitambua mchango muhimu uliotekelezwa na nchi hizo.

Kenya imeahidi kuwa itaendelea kuunga mkono maono ya AU ya kuwa na bara lenye umoja na linalostawi.

Share This Article