Kenya imeunga mkono jitihada zinazoendelea zinazofanywa na nchi za Misri, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Marekani, almaarufu Quad, zinazolenga kurejesha amani nchini Sudan.
Mzozo nchini Sudan unaohusisha jeshi la nchi hiyo na vikosi vyenye hadhi ya kijeshi vya Rapid Support Forces (RSF) umesababisha maafa yasyiyohesabika nchini humo huku hali ya kibinadamu ikiendelea kuzorota.
Kwenye taarifa, Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi amesema jitihada hizo zinaakisi dhamira ya pamoja ya kufanyika kwa mazungumzo yenye kusudi la kurejesha amani ya kudumu nchini Sudan na kanda hiyo kwa jumla.
“Mkutano wa Quad ni jitihanda chanya zinazopaswa kukubaliwa na pande zote kwenye mgogoro nchini Sudan. Janga hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa nchini Sudan linahitaji juhudi za pamoja katika ngazi za taifa, kikanda, na dunia, ambazo zinaweza kuchangia suluhu ya amani,” alisema Mudavadi kwenye taarifa.
“Kenya inaunga mkono jitihada za Quad, ikibaini kwamba wasiwasi wake unawiana na msimamo wa Kenya juu ya Sudan, hasa ukweli kwamba hakuwezi kupatikana suluhu ya kijeshi kwa mgogoro huo.”
Mudavadi ametoa wito kwa pande husika kwenye mgogoro huo ambazo ni jeshi la Sudan na RSF kusuluhisha tofauti zao kupitia mazungumzo.
Kenya pia imekatalia mbali juhudi zozote za kugawa taifa lolote huru na kusisitiza kuunga mkono nchi moja ya Sudan kwa manufaa ya watu wake.
Aidha, imelaani makundi ya yenye itikali kali kwa kuchochea mgogoro huo na ukosefu wa uthabiti wa kikanda na kutaka kusitishwa kwa msaada wa kijeshi kutoka nje kwa nchi hiyo ili kuhakikisha mzozo huo unamalizika.