Huku Wiki ya Unyonyeshaji Duniani (WBW) 2025 ikifikia ukingoni, Kenya imeonyesha tena dhamira yake ya kuhakikisha kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama unachukuliwa kama kipaumbele cha afya ya umma na hatua madhubuti kuchukuliwa kupambana na utapiamlo kwa njia endelevu na jumuishi.
Kaulimbiu ya mwaka huu, “Toa Kipaumbele kwa Unyonyeshaji – Unda Mifumo Endelevu ya Msaada,” iliweka msisitizo mkubwa juu ya umuhimu wa mshikamano na ushirikiano katika jamii nzima—kutoka ngazi ya familia hadi sera za kitaifa na kaunti.
Sherehe za kitaifa za wiki hii zilifanyika rasmi Agosti 5 katika Chuo Kikuu cha Rongo, kaunti ya Migori, ambapo wadau mbalimbali walikusanyika, wakiwemo wawakilishi wa serikali kuu na za kaunti, vyuo vikuu, mashirika ya kiraia, na washirika wa maendeleo.
Katika tukio hilo, kulisisitizwa haja ya kuendeleza unyonyeshaji, kuboresha lishe, na kuunganisha mifumo ya maji, usafi na afya (WASH) ili kuimarisha afya ya mama na mtoto.
Katibu Mkuu wa Afya ya Umma na Viwango vya Kitaaluma, Mary Muthoni, alieleza kuwa unyonyeshaji ni zaidi ya chaguo la binafsi.
Alisema ni jukumu la kitaifa lenye manufaa mapana kiafya, kiuchumi na kijamii.
“Unyonyeshaji si chaguo la kibinafsi tu. Ni kipaumbele cha kitaifa chenye manufaa ya muda mrefu. Tunapaswa kujenga mifumo inayolinda, kusaidia, na kuendeleza unyonyeshaji — nyumbani, kazini, na katika maeneo ya umma,” alisema.
Aidha, alitoa wito kwa sekta mbalimbali, kama vile maeneo ya kazi, vituo vya afya, taasisi za elimu, na jamii kuwekeza katika mifumo ya msaada, akibainisha kuwa mzigo wa malezi haupaswi kubebwa na kina mama peke yao.
Kongamano la kwanza kabisa la Nutri-WASH lilifanyika Agosti 6-7 katika Chuo Kikuu cha Rongo, likiwa mojawapo ya mambo ya kipekee yaliyoibua mjadala wa kitaifa.
Tukio hili lilihudhuriwa na Gavana wa Migori, Dkt. Grace Ochillo, pamoja na wake wa magavana kutoka kaunti za Marsabit, Bungoma, na Bomet.

Washiriki waliwemo wataalamu, watunga sera, watafiti, na wahudumu wa afya waliokuja kuchunguza namna mifumo ya lishe na usafi inaweza kushirikiana ili kupunguza utapiamlo.
Mjadala ulibainisha kuwa upatikanaji wa maji safi, elimu ya usafi wa chakula, na tabia bora za usafi ni msingi muhimu wa kufanikisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama na ukuaji bora wa watoto.
Dkt. Ochillo alisisitiza kuwa suala la lishe lazima liangaliwe kama haki ya binadamu na pia kama ajenda ya kisiasa.
“Utapiamlo si jambo la pembeni, ni suala la kisiasa na haki za binadamu. Ni kuhusu heshima, utu na mustakabali wa watoto wetu,” alisema.
Alitaja pia mafanikio ya kaunti ya Migori katika kupunguza kiwango cha udumavu kutoka 28% hadi 15% kupitia juhudi zinazoongozwa na jamii.

Afisa mmoja wa afya aliongeza kuwa kuna dhana potovu katika baadhi ya jamii ambapo kula vizuri huonekana kama anasa, akisema: “Tunapaswa kuendelea kuwahamasisha wananchi kuwa lishe bora ni msingi, si fahari.”
Mke wa Gavana wa Marsabit, Alamitu Jattani, alieleza kuwa mizizi ya utapiamlo katika eneo hilo ni ujinga, mila potovu, na shughuli za kiuchumi zinazowazuia wakazi kupata chakula chenye virutubisho.
Alisisitiza kuwa ni muhimu kufikisha ujumbe wa lishe kwa njia rahisi ili jamii ziweze kuelewa na kuchukua hatua.
“Tunahitaji kufanya ujumbe wa lishe kuwa rahisi kueleweka. Lishe bora haipaswi kuonekana kama jambo gumu,” alisema.
Kwa upande wake, Bi. Margret Lusaka kutoka Bungoma alisema kuwa utofauti wa kitamaduni unaendelea kuathiri tabia za lishe.
Alisema, “Kadri mtu anavyokuwa maskini, ndivyo anavyofikiri kuwa mkate ni afya.”
Alieleza kuwa watu wengi huona vyakula vilivyosindikwa kama ishara ya ustaarabu, huku wakisahau thamani ya vyakula vya kienyeji ambavyo mara nyingi vina virutubisho bora zaidi.
Mke wa Gavana wa Bomet, Selina Barchok, alibainisha kuwa Bomet ina kiwango cha chini cha utapiamlo kutokana na juhudi zinazotegemea jamii.
Alisisitiza kuwa wanawake wanapaswa kuhakikisha wanapika vyakula bora kwa kutumia kile ambacho wanaume wameleta, huku akitoa wito kwa wanaume kutoachia jukumu hilo kwa wake zao pekee.
Pia alitaja kuwa kaunti yao inasambaza mbegu za mboga na aina maalum ya maharagwe kwa kina mama waliopata watoto ili kuboresha lishe ya familia.

Hata hivyo, alielezea changamoto ya vijana kupuuza mboga za kienyeji kama managu, terere na sagaa akisema, “Vijana wa siku hizi ni wagumu sana kula mboga hizi. Watoto hufuata wanachoona, si wanachoambiwa. Sio bora chakula, ni chakula bora.”
Dkt. Joyce Apuka, daktari wa watoto katika Hospitali ya Rufaa ya kaunti ya Migori, alieleza kuwa kuna ongezeko la mama wachanga chini ya umri wa miaka 25 ambao hawajajiandaa kulea watoto kwa njia bora.
“Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanaingia hospitalini wakiwa katika hali mbaya sana, mara nyingi ikiwa ni kuchelewa,” alisema, akihimiza kuwa Wasaidizi wa Afya wa Jamii wapatiwe mafunzo, vifaa, na msaada wa kutosha ili kusaidia familia mapema kabla hali kuwa mbaya.
Katika hotuba yenye msisimko, Mkurugenzi wa shirika la CARE Kenya, Hellen Owiti, alieleza kuwa hali halisi ya wanawake haizingatiwi vya kutosha katika sera nyingi.
“Tunabuni sera kuhusu wanawake bila kuwahusisha. Tunahimiza unyonyeshaji bila kuwapa maeneo salama au maji safi,” alisema.
Aliongeza kuwa utapiamlo na ukosefu wa usafi wa mazingira ni dalili ya jamii kutoona thamani ya kazi zisizolipwa za wanawake.
Alielezea mafanikio ya CARE Kenya kupitia mifano kama Shule za Mashamba na Biashara, Vikundi vya Akiba na Mikopo (VSLA), na Vikundi vya Mama kwa Mama, ambavyo vimekuwa vikitumika kuwawezesha wanawake, kukuza lishe bora, na kuongeza uthabiti wa familia.
Aliangazia mafanikio mbalimbali kama vile asilimia 60 ya nafasi katika kamati za maji kaunti ya Garissa kushikiliwa na wanawake, kuwekwa kwa vyumba vya kunyonyesha katika hospitali za rufaa za kaunti za Nakuru na Nyandarua, na wanawake katika kaunti ya Homa Bay kuwa na usemi mkubwa katika matumizi ya bajeti za kaya.
Licha ya mafanikio hayo, alionya kuwa ukosefu wa uratibu wa sera na fedha ni changamoto kubwa.
“Uhalisia wa wanawake si kikwazo,” alisema. “Ni ramani ya kujenga mifumo bora.”
Katika wiki hii ya maadhimisho, ilibainika kuwa kaunti 14 kati ya 47 nchini Kenya zinaathirika kwa kiasi kikubwa na utapiamlo, jambo ambalo linaonyesha kuwa utapiamlo si tu suala la afya ya umma bali pia ni tatizo la kijamii, kisiasa, na kiuchumi linalohitaji suluhisho la kina.
Wazungumzaji wengi walisisitiza kuwa mabadiliko ya tabia, uongozi shirikishi, na nia ya kisiasa ni muhimu katika kushughulikia mizizi ya matatizo ya lishe.
Ilipendekezwa kuwa wanaume wanapaswa kushirikishwa katika utoaji wa chakula na malezi ya familia, na mama wa umri mdogo wanahitaji elimu na msaada maalum.
Kwa upande mwingine, wasaidizi wa afya ya jamii wanahitaji mafunzo na rasilimali za kutosha ili kuongoza mabadiliko ya tabia katika jamii.
Pia, utofauti wa lishe, uwekezaji katika miundombinu ya usafi wa mazingira, na uundaji wa maeneo rafiki kwa unyonyeshaji kazini na katika jamii ni hatua muhimu zilizosisitizwa.