Rais William Ruto, ametoa wito wa kufanywa marekebisho katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ili kuliwezesha kukabiliana na changamoto ibuka duniani.
Kulingana na Rais Ruto, mfumo wa sasa wa baraza hilo umeshindwa kushughulikia majanga kama vile Mabadiliko ya Tabia Nchi, ukosefu wa usawa, madeni na mizozo.
Kiongozi huyo wa taifa alisema mfumo huo wa sasa haujatoa suluhu kwa changamoto zilizopo kwa wakati ufaao.
“Bila kuwepo kwa hatua za haraka, binadamu watakabiliwa na majanga ya kimataifa,” alisema Rais Ruto.
“Hatuna budi kutupilia mbali mifumo iliyopitwa na wakati, na kubuni mikakati ya ushirikiano wa kimataifa itakayowafaidi watu bilioni nane,” aliongeza Rais Ruto.
Rais aliyasema hayo alipohutubia mkutano kuhusu mustakaba, katika ukumbi wa Umoja wa Mataifa, Jijini New York Marekani.
Rais Ruto yuko nchini Marekani kuhudhuria mkutano wa 79 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,UNGA79