Kenya yashindwa kibabe na Morocco,AFCON U20

Kwa jumla, Morocco walikuwa na mashambulizi 23 huku tisa yakilenga goli la Kenya, wakati Kenya wakipiga mashambulizi 17, saba yakilenga goli la Morocco.

Dismas Otuke
2 Min Read

Timu ya Kenya kwa chipukizi walio chini ya umri wa miaka 20 almaarufu Rising Stars, ilianza vibaya fainali za kombe la AFCON kwa kipigo cha mabao 3-2 na Morocco, katika kundi B Alhamisi usiku ugani 30th June Air Defence jijini Cairo, Misri.

Kenya walidhihirisha mchezo mzuri tokea mwanzo hadi mwisho huku wakitangulia kufunga goli kunako dakika ya 16 kupitia kwa Lawrence Ouma, aliyepokea pasi kutoka kwa Kevin Wanganya.

Morocco walisawazisha mwishoni mwa kipindi cha kwanza kupitia kwa Yassir Zabiri, na kipindi cha kwanza kimalizikia sare ya 1-1.

Hata hivyo, Kenya walishindwa kuondosha mpira wa ikabu karibu na lango lao na kumruhusu Zabiri kuwaweka Morocco uongozini dakika ya 55.

Rising Stars walijizatiti kwa mashambulizi ya kushtukiza yaliyozaa matunda baada ya Adrien Kibet, kumpokeza pasi Hassan Beja aliyetikisa nyavu dakika ya 71 .

Dakika saba baadaye Kenya walishindwa kuondosha shambulizi langoni mwao na kumruhusu Reda Laalaouwi, kuwarejesha Young Atlas, uongozini kwa bao la tatu.

Morocco walipata penati mwishoni mwa mechi ambayo iliyopanguliwa na kipa Benard Jairo, na hadi kipenga cha mwisho Morocco wakishinda 3-2.

Kenya watarejea uwanjani Jumapili hii dhidi ya Tunisia, kabla ya kuhitimisha ratiba dhidi ya mabingwa mara saba Nigeria Mei, 7.

Kwa jumla, Morocco walikuwa na mashambulizi 23 huku tisa yakilenga goli la Kenya, wakati Kenya wakipiga mashambulizi 17, saba yakilenga goli la Morocco.

Share This Article