Kenya yashauri raia wake walio Israel na Iran

Nchi hizo mbili zimekuwa zikishambuliana hali inayozidi kuwa mbaya.

Marion Bosire
2 Min Read
Roseline Njogu, Katibu wa Masuala ya Ughaibuni

Wizara ya masuala ya kigeni nchini Kenya imetoa ushauri wa dharura kwa raia wake walioko nchini Israel na nchini Iran huku mvutano kati ya nchi hizo mbili ukiendelea kuongezeka.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatano, idara ya masuala ya ughaibuni imesihi wakenya hao wawe waangalifu sana, waepushe safari zisizo za lazima na wafuatilie taarifa za habari za nchi hizo na maonyo ya dharura yatakayotolewa.

Raia hao wa Kenya wamehimizwa pia kufuata maelekezo ya mamlaka za karibu katika maeneo waliko ili kupata bidhaa muhimu na hati.

“Lengo letu kuu ni usalama wa wakenya ugaibuni” alisema katibu wa masuala ya ughaibuni Roseline Kathure Njogu katika taarifa hiyo huku akiwakumbusha walengwa wa taarifa hiyo wadumishe mawasiliano na familia zao humu nchini na afisi za ubalozi za Kenya nchini Iran na Israel.

Idara hiyo ilitoa anwani za mawasiliano za balozi za Tel Aviv na Tehran kwa wale wanaotaka usaidizi na kuwaambia wajisajili katika balozi hizo iwapo bado hawajajisajili ili kufanikisha usaidizi na hata usafiri wao.

Nambari ya simu ya idara hiyo ya masuala ya ughaibuni jijini Nairobi ni +254 20 7876000 na anwani ya barua pepe ikiwa consular@diaspora.go.ke.

Serikali ya Kenya imetoa ahadi ya kuendelea kufuatilia hali katika nchi hizo mbili kwa karibu na kusisitiza kujitolea kwake kulinda raia wake ughaibuni.

Share This Article