Kenya yapongeza makubaliano ya kusitisha mzozo kati ya Israel na Hamas

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi.

Kenya imekaribisha awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na Hamas, ikitaja hatua hiyo kuwa muhimu katika kumaliza mateso Gaza.

Kupitia kwa taarifa siku ya Alhamisi, Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, alisema inakaribisha makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka wa Israel na Palestina, uondoaji wa vikosi vya ulinzi na kufanikisha uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu Gaza.

“Kenya inakaribisha awamu ya kwanza ya makubaliano ya kumaliza vita kati ya Israel na Hamas,” alisema Mudavadi kwenye taarifa.

Mudavadi aliyepia Waziri wa Mambo ya Nje, alituma rambirambi kwa familia za waliopoteza jamaa wao kwenye mzozo huo.

Mudavadi alidokeza kuwa makubaliano hayo yanawiana na msimamo wa Kenya jinsi ulivyowasilishwa na Rais William Ruto wakati wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka 2024.

“Kenya inapigia debe suluhu la kudumu unaowaruhusu watu wa Gaza, Israel na kanda ya Asia kuishi kwa amani,” alisema Mudavadi.

Mudavadi aliwashukuru wapatanishi wa mzozo huo, kwa wajibu muhimu waliotekeleza kuhakikisha amani inapatikana.

“Tunapongeza Marekani, Misri, Qatar na Uturuki kwa jukumu kubwa la kumaliza mzozo huo.,” aliongeza Mudavadi.

Share This Article