Kenya yanakili vifo 2,933 kufuatia ajali za barabarani 2025

Tom Mathinji
2 Min Read
Watu 2,933 wamefariki kwenye ajali za barabarani hapa nchini tangu mwezi Januari.

Vifo kutokana na ajali za barabarani vimeongezeka hapa nchini huku watu 2,933 wakipoteza maisha yao tangu mwezi Januari, 2025, kulingana na takwimu zilizotolewa na Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir.

Takwimu hizo zinaibua wasiwasi, baada ya ajali 80 kunakiliwa katika muda wa siku nne zilizopita zinazohusisha magari ya umma na ya kibinafsi na yale ya kibiashara.

Waziri Chirchir, ametangaza kuwa kundi la asasi mbalimbali zimetumwa kukadiria hali ilivyo kwenye barabara za humu nchini na kuchukua hatua mwafaka.

Amesema kundi hilo linatarajiwa kukamilisha zoezi hilo katika muda wa siku saba na kuwasilisha mapendekezo ya kiufundi ili hatua za haraka zichukuliwe kuepusha maafa zaidi.

“Kama wizara, tutaendelea kushirikiana na wadau kutekeleza mikakati ya muda mfupi na ile ya muda mrefu kuambatana na mpango wa kitaifa wa usalama barabrani wa kati ya mwaka 2024 hadi 2028,” alisema Chirchir.

Hatua hiyo inajiri baada ya watu 26 kufariki baada ya basi walimokuwa wakisafiria kubingiria na kuanguka mtaroni kwenye mzunguko wa Coptic kwenye barabara ya Kisumu-Kakamega Ijumaa wiki iliyopita.

Saa chache baadaye, watu wengine wanane waliangamia kwenye ajali nyingine ya barabarani katika eneo la Korompoi kwenye barabara ya Kitengela-Isinya, huku wito ukitolewa kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuzuia ajali zaidi.

Wakati huo huo, Waziri huyo alituma risala za rambirambi kwa familia zilizowapoteza wapendwa wao, akiwatakia afueni ya haraka waliojeruhiwa kufuatia ajali za barabarani kote nchini.

Share This Article