Kenya yalaani shambulizi la Israel nchini Qatar, Israel yatishia kuua viongozi zaidi wa Hamas

Martin Mwanje
3 Min Read
Musalia Mudavadi - Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya

Kenya imeungana na mataifa mengine ya ulimwengu kulaani shambulizi la bomu la Israel nchini Qatar lililosababisha maafa na uharibifu wa mali. 

Sshambulizi hilo la juzi Jumanne jijini Doha lilisababisha vifo vya watu wasiopungua sita.

Kwenye taarifa leo Alhamisi, Wizara ya Mambo ya Nje imesema shambulizi hilo linatishia usalama wa taifa hilo la ghuba na amani ya dunia.

“Kwa kukiri yenyewe, nchi ya Israel ilitekeleza shambulizi hilo la bomu,” ilisema taarifa hiyo iliyolalamikia vifo vilivyotokea, uharibufu wa mali na ukiukaji wa uhuru wa Qatar.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kitendo kama hicho kinakiuka sheria ya kimataifa na kudhoofisha kanuni za kuishi kwa amani kama ilivyoelezwa katika Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya Uhusiano wa Kirafiki miongoni mwa mataifa.

Kenya sasa inatoa wito kwa nchi zote na jumuiya ya kimataifa kujizuia na kushiriki mazungumzo badala ya kuzidishia mgogoro huo.

Taarifa hiyo imekuja wakati ambapo Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ametishia kuwaua tena viongozi wa Hamas walioko nchini Qatar iwapo Doha haitawafukuza maafisa hao, na kusababisha majibu makali kutoka kwa serikali ya Qatar.

Pamoja na ukosoaji huo wa kimataifa kuhusu shambulizi lililotokea katika mji mkuu wa Qatar, inaarifiwa kuwa Netanyahu hajatetereshwa kwa namna yoyote.

Netanyahu alisema siku ya Jumatano kwamba mataifa yanapaswa “kuipongeza” Israel kwa mashambulizi yake ya mabomu na mauaji katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati.

Kauli hizo zilitolewa siku moja baada ya Israel kufanya shambulio lisilo la kawaida ndani ya Qatar, kwa kuwalenga viongozi waandamizi wa Hamas walioko Doha, wakati mazungumzo kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano lililoungwa mkono na Marekani yakiendelea.

Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imelaani vikali kauli za Waziri Mkuu huyo wa Israeli, ikizitaja kama “jaribio la aibu … la kuhalalisha shambulio la kinyonge dhidi ya ardhi ya Qatar, pamoja na vitisho vya wazi vya kuvunja tena mamlaka ya kitaifa ya nchi.”

“Netanyahu anafahamu vyema kuwa ofisi ya Hamas ilifunguliwa nchini Qatar katika muktadha wa juhudi za upatanishi zilizopigiwa chapuo na Marekani pamoja na Israel,” Taarifa hiyo imeeleza.

“Kauli kama hizi si jambo la kushangaza kutoka kwa mtu anayejiegemeza katika misimamo mikali ili kupata ushindi wa kisiasa, huku akiwa anatafutwa na vyombo vya sheria za kimataifa, akikabiliwa na vikwazo vinavyozidi kuongezeka kila uchao hali inayozidi kumtenga katika jukwaa la kimataifa,” Taarifa hiyo iliongeza.

Wakati hayo yakijiri, ikumbukwe kwamba ndani ya kipindi cha siku tatu pekee, Israel imefanya mashambulizi katika maeneo ya Gaza, Lebanon, Yemen, Syria, Tunisia na Qatar, huku ikiendeleza uvamizi wa kila siku katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na siku ya Jumatano, Israeli iliwaua watu 35 katika shambulio nchini Yemen.

Share This Article