Waandamanaji wameushambulia ubalozi wa Kenya katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC.
Waandamanaji hao pia wameushambulia balozi kadhaa ikiwa ni pamoja na ubalozi wa Ufaransa mjini Kinshasa, ule wa Uganda na Afrika Kusini katika hatua ya kulalamikia mgogoro unaorindima mashariki mwa DRC.
Katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya Korir Sing’oei amelaani mashambulizi hayo akiyataja kuwa ukiukaji wa sheria ya kimataifa.
“Tuna mashaka makubwa kutokana na uzingiraji na mashambulizi yanayoendelea kwenye majengo ya balozi mjini Kinshasa, DRC, ikiwa ni pamoja na balozi za Kenya, Uganda na Afrika Kusini, yanayofanywa na waandamaji wanaoelezea malalamiko yao juu ya mgogoro upande wa mashariki mwa nchi hiyo,” alisema Sing’oei katika taarifa.
“Hatua hii ni ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa na tunailani vikali mno.”
Sing’oei sasa anatoa wito kwa mamlaka nchini DRC kuchukua hatua stahiki akiongeza kuwa Kenya inasimama sako kwa bako na taifa hilo wakati huu mgumu na itatumia njia zote za kidiplomasia kufanya kazi na eneo hili kutafuta amani ya kudumu nchini humo.
Hayo yanajiri wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot pia amelaani shambulizi dhidi ya ubalozi wa Ufaransa mjini Kinshasa na waandamanaji leo Jumanne asubuhi.
“Mashambulizi haya hayakubaliki,” alisema kwenye mtandao wa X akiongeza kwamba waandamanaji “walisababisha moto ambao sasa umedhibitiwa”.
Moshi mwingi ulionekana ukifuka kutoka kwa ubalozi wa Ufaransa, baada ya sehemu yake kuchomwa moto.
“Kila kitu kinafanywa ili kuhakikisha usalama wa mawakala wetu na raia,” Barrot aliongeza.
Waandamanaji pia walilenga balozi za Rwanda, Ubelgiji, Uholanzi na Marekani.
Taarifa hii imechangiwa na BBC