Kenya yajiunga na OSS kama makamu wa rais wa tatu

Marion Bosire
2 Min Read

Kenya imejiunga rasmi na Bodi ya Shirika la uangalizi la Sahara na Sahel (OSS) kama makamu wa tatu wa rais, wadhifa muhimu wa uongozi unaodhihirisha tena dhamira ya nchi hii ya kuimarisha ushirikiano wa kimazingira wa kikanda na uimara dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Tangazo hili lilitolewa Jumatano katika mkutano wa Bodi ya OSS.

Akizungumza baada ya tangazo hilo, Katibu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi Festus Ng’eno, anayewakilisha Kenya kwenye mkutano huo, alisema wadhifa huo mpya wa uongozi inaimarisha sauti ya Kenya katika kuunda mikakati ya usimamizi endelevu wa ardhi na maji katika eneo la Sahel na Sahara.

“Tunasubiri kwa hamu kushirikiana na nchi wanachama kuendeleza hatua za pamoja za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kurejesha mifumo ya ikolojia barani Afrika” alisema Ng’eno.

Wadifa wa mwenyekiti ulichukuliwa na Misri, huku Ufaransa, Libya, Benin na Mauritania zikiwa makamu wa Kwanza, wa Pili na wa Nne mtawalia.

OSS ilianzishwa mwaka 1992 na imekuwa na makao yake makuu jijini Tunis tangu mwaka 2000, ikiwa shirika la kimataifa linalolenga bara la Afrika.

Dhamira yake ni kuendeleza na kusaidia ushirikiano unaokabiliana na changamoto kuu za kimazingira kama vile usimamizi wa rasilimali za maji, mmomonyoko wa ardhi, uhifadhi wa bayoanuwai na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa sasa, OSS ina wanachama 28 kutoka Afrika na 7 kutoka nje ya Afrika, pamoja na mashirika 12 yanayowakilisha Afrika Magharibi, Mashariki na Kaskazini, pamoja na mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa na asasi zisizo za kiserikali.

Ushirikiano huu unalenga kuimarisha juhudi za pamoja kwa ajili ya mustakabali endelevu wa eneo hili.

Dhamira ya OSS ni kusaidia nchi za Afrika wanachama kusimamia rasilimali zao asilia kwa njia endelevu, hasa katika muktadha mgumu wa mabadiliko ya tabianchi.

Shughuli zake zinazingatia maeneo kame, nusu-kame na yenye unyevunyevu wa wastani barani Afrika.

Nafasi mpya ya uongozi ya Kenya katika Bodi ya OSS inatarajiwa kuimarisha ushawishi wake katika kuendeleza ajenda ya sera za mazingira barani Afrika na kuchangia maendeleo endelevu katika mifumo ikolojia inayokabiliwa na changamoto katika eneo hili.

Share This Article