Kenya yajipatia nafasi kwenye kamati ya INTERPOL Afrika

Haya yanafuatia kuchaguliwa kwa raia wa Kenya Ibrahim Jillo kama mjumbe wa kamati ya INTERPOL Afrika kwa kura nyingi kutoka kwa nchi wanachama.

Marion Bosire
1 Min Read

Taifa la Kenya limepata mafanikio makubwa katika kamati ya shirika la maafisa wa polisi wa kimataifa almaarufu Interpol katika bara Afrika.

Haya yanafuatia kuchaguliwa kwa raia wa Kenya Ibrahim Jillo kama mjumbe wa kamati ya INTERPOL Afrika kwa kura nyingi kutoka kwa nchi wanachama.

Jillo ambaye ni mkurugenzi wa afisi Kuu ya kitaifa (NCB)–Kenya, alichaguliwa katika mkutano wa 27 wa kamati hiyo ya INTERPOL ya Kanda ya Afrika uliofanyika katika jiji la Cape Town, nchini Afrika Kusini.

Bwana Jillo atahudumu kwa kipindi cha miaka minne katika Kamati hiyo, akiiletea Kenya heshima na kuchangia katika maamuzi muhimu ya kupambana na uhalifu wa kimataifa, ugaidi, na uhalifu wa kifedha barani Afrika.

Uchaguzi huu unaonyesha imani kubwa kwa uongozi wa Kenya na kujitolea kwake kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika utekelezaji wa sheria.

Shirika la INTERPOL ndilo shirika kubwa zaidi la polisi ulimwenguni na lilibuniwa 1923 kufanikisha ushirikiano kati ya maafisa wa polisi ulimwenguni na uthibiti wa jinai katika nchi 196 wanachama.

INTERPOL hutoa mtandao thabiti wa mawasiliano wa kushiriki habari, kudumisha hifadhideta ya ulimwengu kuhusu uhalifu na wahalifu na usaidizi katika uchunguzi.

Share This Article