Kenya inajizatiti kukabiliana na Saratani ya mlango wa uzazi, huku ikitarajiwa kuzindua matumizi kamili ya chanjo ya HPV mwezi Oktoba mwaka huu.
Akizungumza Jumatano wakati wa ufunguzi wa kongamano la muungano wa kuhimiza matumizi ya chanjo hiyo hapa nchini, Mkurugenzi wa Matibabu Dkt. Patrick Amoth, alisema hatua hiyo ilitokana na mapendekezo ya kamati ya ushauri ya kitaifa kuhusu chanjo, ambayo ilipendekeza matumizi ya dozi moja ya chanjo hiyo badala ya tembe.
Dkt. Amoth alisema matumizi ya chanjo hiyo ni ya gharama nafuu na yataiweka Kenya kwenye mstari wa mbele wa uvumbuzi wa kimatibabu.
Kwa sasa saratani hiyo ya njia ya uzazi imekithiri miongoni mwa wanawake nchini huku ikisababisha vifo vya wanawake kumi kila siku.
Wataalam wa afya wameonya kuwa endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa,idadi hiyo huenda ikaongezeka marudufu kufikia mwaka 2040.
Kongamano hilo la siku tatu liliwaleta pamoja wajumbge kutoka mataifa 20 ya Afrika zikiwemo Kenya, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Cote D’Ivoire, DRC Congo, Ethiopia, Gambia, Guinea, Malawi, Mali, Mozambique, Nigeria, Rwanda, Senegal, Siera Leone, Afrika Kusini, Tanzania, Uganda and Zimbabwe.
Kongamano hilo liliungwa mkono na wakfu wa Bill and Melinda Gates,shirika la Jhpiego pamoja na wadau wengine wa kimataifa.