Kenya imetoa wito wa mbinu jumuishi na ya haki zaidi katika usimamizi wa kimataifa wa teknolojia ya akili unde – AI katika mkutano wa ngazi za juu wa mashauriano ya wadau mbalimbali kuhusu mjadala wa kimataifa wa usimamizi wa AI katika Umoja wa Mataifa, UN.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi Dijitali William Kabogo alisisitiza msimamo wa Kenya kwamba UN inabaki kuwa jukwaa kuu la kuongoza mustakabali wa teknolojia za mageuzi, hasa kwa mataifa yanayoendelea duniani.
“Kenya imesisitiza kwamba Umoja wa Mataifa lazima ubaki kuwa jukwaa la kimataifa ambapo mataifa yote… yanaweza kushiriki katika kuunda mifumo ya usimamizi wa teknolojia za mageuzi kama vile akili unde,” alisema Kabogo.
Alielezea hatua zilizopigwa na Kenya katika maendeleo ya AI na teknolojia ya kidijitali, ikiwemo Mkakati wa Kitaifa wa AI 2025–2030, sheria madhubuti za ulinzi wa data na usalama wa mitandao, pamoja na sera zijazo za Usimamizi wa AI na Data.
Ajenda ya Kenya ya Miundombinu ya Umma ya Kidijitali inalenga kuhakikisha huduma zinazotumia AI zinapatikana kwa wote, zinaaminika na ni jumuishi.
Kabogo alirudia wito wa Rais William Ruto wa kufanya mageuzi ya kifedha ya kimataifa ili kuhakikisha uwezo wa AI, ikiwemo data, nguvu ya kompyuta, ujuzi na taasisi, unasambazwa kwa usawa.
“Ufadhili wa teknolojia lazima uwe wa haki zaidi na wenye utabiri,” alisisitiza Kabogo, akionya dhidi ya maendeleo ya AI kuachwa mikononi mwa mataifa machache yaliyoendelea.
Kenya imeahidi kushirikiana na washirika wa kimataifa kujenga mfumo wa AI unaozingatia utu, uwajibikaji na usawa.
Mashauriano hayo ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kuunda mfumo wa pamoja wa usimamizi wa AI, kabla ya mazungumzo rasmi yanayotarajiwa ndani ya mfumo wa UN.