Kenya na Uganda zimetia saini Mikataba mipya minane ya Maelewano (MoUs) kwa lengo la kuboresha uhusiano wa muda mrefu uliodumu kati ya nchi hizo.
Hafla ya kutia saini mikataba hiyo ilifanyika katika Ikulu ya Nairobi wakati wa ziara ya Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni humu nchini.
Rais William Ruto anasema utiaji saini mikataba hiyo utachochea zaidi maendeleo ya kiuchumi kati ya nchi hizo.
“Kenya na Uganda zina ushirikiano wa kihistoria uliojikita kwenye mawazo sawa, heshima ya dhati, na dhamira ya pamoja ya uthabiti na ustawi wa kikanda,” alisema Rais Ruto aliyefanya mazungumzo na Rais Museveni katika Ikulu ya Nairobi.
“Utiaji saini wa Mikataba mipya minane ya Maelewano siyo tu kwamba utaimarisha ushirikiano wetu, bali pia utachochea maendeleo ya kiuchumi, kuboresha uhusiano baina ya watu, na kuhakikisha uhusiano wetu unaleta manufaa yaliyo dhahiri kwa raia wetu.”

Wakati wa mazungumzo baina yao, viongozi hao wawili walizungumzia ujenzi wa reli ya Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Naivasha kuelekea Malaba hadi nchini Uganda na ujenzi wa barabara ya pande mbili ya Nairobi-Nakuru-Mau Summit.
Barabara hiyo hatimaye itajengwa hadi Malaba na nchini Uganda.
“Tulikubaliana kuangazia changamoto za mpakani ikiwa ni pamoja na suala la uvuvi katika kisiwa cha Migingo,” alisema Rais Ruto.