Kenya Simbas yapigwa butwaa na Algeria Raga ya Afrika

Dismas Otuke
2 Min Read

Timu ya raga ya Kenya kwa wachezaji 15 kila upande maarufu kama  Simbas wamemaliza kampeni yao katika mashindano ya Kombe la Afrika ya mchezo wa raga, 2025 Rugby Africa Cup , vibaya baada ya kukubali kichapo cha 15-5 kutoka kwa Algeria, kwenye mchezo uliopigwa Mandela National Stadium, nchini Uganda.

Kichapo hicho, kimetonesha kidonda cha Kenya dhidi ya Algeria, kwani katika makala ya mwaka jana, itakumbukwa kuwa, Simbas walibanduliwa katika hatua ya nusu fainali, kwa kipigo cha 20-12.

Algeria, walianza kutawala mchezo kuanzia dakika ya kwanza, wakiwaduwaza vijana wa mkufunzi Jerome Paarwater kwa kufunga try ya haraka. Simbas walijibu mapigo katika dakika ya 9, baada ya vuta nikuvute iliyoshuhudia Teddy Akala, akivuka mstari na kusawazisha.

Hata hivyo, jaribio la Brian Wahinya kupiga ‘Conversion’ halikuzaa matunda baada ya mpira kupaa juu. Licha ya kuingioa kwenye mchezo wa leo, wakiwa na rekodi nzuri kutokana na kufunga penalti kadhaa, Kenya Simbas hawakufua dafu mbele ya Algeria.

Katika dakika ya 20, Algeria walitumia vyema makosa ya mabeki wa Kenya, kufunga Try, iliyowahikishia kwenda mapumziko wakiwa vifua mbele na ushindi wa 12-5.

Kipindi kilianza vizuri kwa upande wa Kenya, wakionesha kutawala mchezo, lakini kutoka na ugumu wa ngome ya ulinzi ya Algeria, haikuwa rahisi kupenya.

Katika kutafuta mbinu ya kutuliza mzuka wa Algeria, Kocha Jerome Paarwater, alifanya mabadiliko ya kikosi, akitoa wachezaji nane na kuleta nguvu mpya, ambao ni pamoja na Wilhite Muhutsi, Andycolle Omollo, Thomas Okeyo, Samuel Asati, Barry Young, Eugene Sifuna, Ephraim Bwire, na Walter Okoth.

Licha ya mabadiliko hayo, Algeria iliendelea kuishambulia Simbas, ambapo katika dakika ya 60 na 77, mikimbio yao ilizaa penalti mbili ambayo hata hivyo haikuzalisha magoli, ikawa ni afueni kwa Simbas. Algeria iliendeleza mashambulizi yaliyowahikishia ushindi wa 15-5.

 

Share This Article