Rais William Ruto amesema Kenya na Uingereza zimeanzisha upya uhusiano wa kimkakati na kutoa fursa kwa ukuaji wa biashara, uwekezaji pamoja na ushirikiano katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Kulingana na kiongozi wa taifa, makubaliano hayo pia yanalenga kuimarisha malengo ya maendeleo, na usalama wa Kikanda ambayo yako kwenye mpango wa mwaka 2020–2025 yalioafikiwa kufuatia mkutano kati yake na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer jijini London.
Rais Ruto alisema makubaliano hayo mapya yanatarajiwa kuimarisha biashara kati ya Kenya na Uingereza katika kipindi cha miaka mitano. Aliongeza kwamba ushirikiano huo utafanikisha uchumi wa kidijitali.
“Kwa lengo la kuongeza maradufu biashara kati ya nchi hizi mbili kwa muda wa miaka mitano ijayo, tuna hakika ushirikiano wetu utafanikisha ukuaji wa uchumi kwa watu wetu,” alisema Rais Ruto.
Kuhusu mradi wa reli wa Jijini Nairobi, Rais alisema utaleta mabadiliko katika sekta ya uchukuzi na kuimarisha uchumi pamoja na ustawi.
Wakati wa mkutano huo, Rais Ruto pia alipongeza ushirikiano kati ya mataifa haya mawili kuhusiana na amani katika kanda hii pamoja na ulinzi akisema mkataba wa ulinzi kati ya Kenya na Uingereza ndio nguzo kuu.