Rais William Ruto amezuru Misri wakati Kenya na Misri zinaadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia, huku viongozi wa nchi hizo mbili wakiahidi kuimarisha uhusiano huo hata zaidi.
Kiongozi wa nchi alikutana na Rais Abdel Fattah El-Sisi na viongozi wengine na alishukuru kwa mapokezi mema aliyopata pamoja na ujumbe wake.
Viongozi hao wawili wametangaza kuanzishwa kwa awamu nyingine ya ushirikiano unaolenga kuimarisha hata zaidi uhusiano wa kiuchumi, kidiplomasia na kiusalama.
Kenya na Misri zimetia saini mikataba 12 ya maelewano hii leo inayogusa sekta mbali mbali kama vile usalama wa baharini, nishati mbadala, uwezeshaji wa vijana na elimu ya juu.
Rais Ruto aliangazia uwezo wa ukuaji wa ubadilishanaji katika biashara, uwekezaji na teknolojia akisisitiza umuhimu wa kuunda mazingira faafu na yenye kutabirika ya biashara.
Ili kuwezesha hayo, Rais alipendekeza uzinduzi wa baraza la pamoja la biashara la Kenya na Misri.
Kuhusu usalama wa kikanda, viongozi wote walithibitisha kujitolea kwao kuhakikisha amani hasa katika maeneo yanayokumbwa na vita huko Mashariki ya kati na Afrika.
Rais Ruto alipongeza Misri kwa juhudi za kuleta uthabiti huko Gaza, Somalia, Sudan na Sudan Kusini.
Kadhalika Kenya na Misri zimeahidi kuendelea kushirikiana na Umoja wa Afrika na mashirika mengine ya kikanda.
Ziara ya Rais Ruto iliangazia umuhimu wa wakenya wanaoishi Misri huku viongozi wa nchi hizo wakitambua mchango wa wataalamu mbali mbali toka Kenya, wanafunzi na hata wanabiashara kwa maendeleo ya Kenya.
Uwaniaji wa Raila Odinga wa uenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika AUC nao uliangaziwa ambapo Rais Ruto aliomba uungwaji mkono wa Misri ili kuhakikisha uongozi dhabiti katika Umoja wa Afrika na mageuzi ya haraka ya kuimarisha mashirika yake.