Rais William Ruto, siku ya Alhamisi, alishuhudia kutiwa saini kwa Mpango wa kihistoria wa Ushirikiano kuhusu afya kati ya Kenya na Marekani, na kuashiria mwanzo wa ushirikiano wa miaka 25 unaolenga kuimarisha Huduma ya Afya kwa wote (UHC) nchini Kenya.
Chini ya mpango huo, Marekani itatoa dola bilioni 1.6 kwa Kenya kwa muda wa miaka mitano ijayo, ambazo zitawasilishwa kupitia taasisi za serikali.
Mkataba huo wa Makabiliano ulitiwa saini na Waziri mwenye Mamalaka Makuu Musalia Mudavadi na waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, na kuchukua mahala pa mkataba wa awali uliotekelezwa na Shirika la Kimataifa la Marekani kuhusu Maendeleo (USAD), lililovunjiliwa mbali mapema mwaka huu.
Kenya inakuwa taifa la kwanza barani Afrika kutia saini makubaliano hayo.
Waziri Rubio alisema mkataba huo na Kenya unalenga kuimarisha uongozi wa Marekani duniani katika sekta ya afya, huku akipongeza mfumo wa afya wa Kenya akisema ni wa kupigiwa mfano.
Mpango huo unalenga kutokomeza ugonjwa wa HIV/AIDS, Kifua Kikuu, Malaria na magonjwa ibuka ya kuambukizana.
Rais William Ruto alitaja hatua hiyo kuwa inayoleta mageuzi.
“Mpango huo unatoa kipaumbele kwa usambazaji wa vifaa vya matibabu kwa hospitali, kuimarisha nguvukazi katika ekta ya afya na kupanua bima ya afya kuhakikisha kila mkenya analindwa,” alisema Rais Ruto.