Kenya na California zaimarisha ushirikiano kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Tom Mathinji
2 Min Read
Kenya na Amerika zashirikiana kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi.

Kenya na jimbo la California nchini  Marekani zimeimarisha ushirikiano katika masuala ya ubunifu, uendelevu, mabadiliko ya tabia nchi, nishati safi na teknolojia.

Akizungumza alipokutana na ujumbe wa mawaziri wa serikali ya jimbo la California pamoja na wadau wa sekta ya kibinafsi kutoka eneo hilo, wakiongozwa na Waziri wa Uchukuzi wa jimbo hilo Toks Omishakin, Rais William Ruto alisema sekta ya teknolojia katika jimbo la California pamoja na juhudi za jimbo hilo za kukabili mabadiliko ya tabia nchi kwa kushirikiana na wafanyakazi waliohitimu kidijitali humu nchini, zinaweza kubuni nafasi kwa ushirikiano zaidi wa kina kati ya jimbo hilo na Kenya.

Ruto amesema Kenya ipo mstari mbele katika jitihada za kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi, ikiwa na asilimia 93 ya nishati safi kwenye mtandao wake.

“Kenya inaongoza katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, ikiwa na asilimia 93 ya nishati safi, huku ikilenga kuwa na asilimia 100 ya nishati safi kufikia mwaka 2030,” alisema Rais Ruto.

Aliongeza kuwa Kenya na jimbo la Califorinia zinashirikiana kwa karibu katika ubunifu wa nishati safi, mbinu za kisasa za kilimo, utafiti pamoja na matumizi ya magari ya uchukuzi yanayotumia nishati safi.

“Pamoja tunafanikisha mifumo ya nishati safi, mbinu bora za kilimo, utafiti, akili mnemba, na mifumo ya uchukuzi inayotumia kawi safi,” alisema Rais Ruto.

Share This Article