Kenya Kwanza ndio muungano wa wengi bungeni, abainisha Wetang’ula

Martin Mwanje
2 Min Read
Moses Wetang'ula - Spika wa Bunge la Taifa

Muungano unaotawala wa Kenya Kwanza ndio ulio na idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Taifa. 

Spika Moses Wetang’ula amesem muungano huo wa walio wengi una jumla ya wabunge 165 ikilinganishwa na 154 wa Azimio.

Wetang’ula aliweka wazi kuwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, muungano wa Azimio ulikuwa na vyama tanzu 21 na wabunge wengi ikilinganishwa na muungano wa Kenya Kwanza.

Hata hivyo, ubabe wa wabunge wengi wa Azimio ulizimwa baada ya baadhi ya vyama tanzu vya muungano huo kuugura na kujiunga na Kenya Kwanza.

Ni hali hiyo iliyosababisha Azimio kupoteza ubabe wake bungeni.

Wetang’ula alisema hawezi akatoa uamuzi wa ni muungano upi ulio na wabunge wengi bila kuangazia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na makubaliano ya baada ya uchaguzi baina ya vyama na miungano ya kisiasa.

Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo jana Jumanne alimtaka Spika kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo baada ya Mahakama Kuu katika uamuzi wake kubaini ya kwamba ni muungano wa Azimio ulio na idadi kubwa ya wabunge.

Katika uamuzi wake leo Jumatano alasiri, Wetang’ula amesema mahakama haikuelezea hivyo kama inavyodai Azimio.

Odhiambo ameelezea kuwa kama Azimio, watatii uamuzi wa Spika kwa mujibu wa kifungu cha 87 (2) cha kanuni za bunge ila watachukua hatua zaidi ambazo hakuzibainisha kuhusiana na suala hilo.

 

 

 

Share This Article