Rais William Ruto ametangaza kwamba Kenya itakaribisha ujumbe wa ngazi ya juu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa – IFC mapema mwaka ujao, ziara inayotarajiwa kuimarisha majadiliano ya uwekezaji katika miradi muhimu ya miundombinu ya taifa.
Akizungumza mjini Washington D.C. nchini Marekani ambako yuko kwa ziara rasmi, Rais Ruto alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa IFC, Makhtar Diop na kuthibitisha dhamira ya Kenya katika mifumo bunifu ya ufadhili wa maendeleo.
Alisema kwamba hazina mpya ya miundombinu iliyopendekezwa na Kenya imevutia shauku kubwa kutoka kwa washirika wa kimataifa, na kuiweka nchi hii katika nafasi ya uongozi katika ufadhili endelevu wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Rais Ruto alifurahia hatua ya IFC ya kudhihirisha imani katika hazina ya miundombinu, akibainisha kwamba msaada wa IFC utaharakisha utekelezaji wa malengo ya kitaifa ya maendeleo.
“Tunashukuru kwa nia ya IFC kuwekeza na tunatarajia kuupokea ujumbe utakaoongozwa na Makamu wa Rais, Kitengo cha Viwanda, Mohamed Gouled, mapema mwaka ujao,” alisema Rais Ruto.
Ziara hiyo inalenga kuendeleza majadiliano kuhusu uwekezaji katika sekta ya nishati na miundombinu, ikijumuisha mipango ya kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi.
Maeneo mengine muhimu ya ushirikiano ni upanuzi wa barabara kuu, pamoja na uzalishaji na usafirishaji wa umeme wa jotoardhi, maji, na upepo.
Rais alisema ushirikiano kati ya serikali na IFC unaonyesha kuongezeka kwa imani ya kimataifa katika mwelekeo wa kiuchumi wa Kenya na dhamira yake ya maendeleo ya mageuzi.