Kenya itazindua kampeni yake ya kuwania ubingwa wa kombe la CHAN dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Agosti 3, mwaka huu katika mchuano wa kundi A.
Kulingana na ratiba ya michuano iliyotolewa jana na shirikisho la soka barani Afrika, CAF, mchuano huo utasakatwa katika uwanja wa kimataifa Kasarani.
Kenya itachuana na Angola katika mechi yake ya pili Agosti saba na baadaye imenyane na Morocco Agosti 10, na kuhitimisha ratiba ya kundi hilo dhidi ya Zambia tarehe 17 Agosti.
Michuano yote ya Harambee Stars itaandaliwa katika uwanja wa Moi, Kasarani huku michuano mingine ya kundi A ikiandaliwa ugani Nyayo.
Wenyeji wenza Tanzania watafungua dimba hilo katika kundi B, dhidi ya Burkina Faso Agosti 2, katika uwanja wa kitaifa wa Benjamin Mkapa, kabla ya kumenyana na Mauritania tarehe sita na Madagascar siku tatu baadaye.
Taifa Stars watakamilisha ratiba ya kundi hilo dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati tarehe 16 Agosti.
Uganda Cranes ambao ni waandalizi wenza watafungua ratiba ya kundi C dhidi ya Algeria tarehe 4 Agosti uwanjani Nelson Mandela, kabla ya kupimana nguvu na Guinea Agosti 8, na dhidi ya Niger siku tatu baadaye.
Uganda watakamilisha mechi za kundi lao dhidi ya Afrika Kusini tarehe 18 Agosti.
Mabingwa watetezi Senegal watafungua kampeni yao kundini D dhidi ya Nigeria tarehe 5 Agosti, katika uwanja wa Amaan kisiwa Zanzibar, na baadaye wakumbane na Congo Agosti 12.
Simba wa Teranga watamenyana na Sudan katika mechi ya mwisho Agosti 19.
Mechi za kwota fainali zitasakatwa kati ya Agosti 23 na 24, ikifuatwa na nusu fainali tarehe 26 Agosti, huku mchuano wa kuwania nishani ya shaba ukichezwa tarehe 29, na hatimaye fainali Agosti 30, katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.