Kenya itaendelea kuunga mkono AU, aahidi Wetang’ula

Martin Mwanje
2 Min Read
Moses Wetang'ula - Spika wa Bunge la Taifa

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula amesisitiza kujitolea kwa Kenya kuendelea kuunga mkono Umoja wa Afrika (AU) kama mwanachama wake. 

Matamashi yake yanakuja wakati ambapo baadhi ya wabunge wamesikika wakipendekeza kuwa Kenya ipunguze ahadi zake kwa AU na hatimaye ijiondoe kwenye umoja huo.

Hii ni baada ya Waziri Mkuu Raila Odinga Februari 15, 2025 kubwagwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ulioshindwa na Mahmoud Ali Youssouf kutoka Djibouti.

Akizungumzia uchaguzi huo, Wetang’ula amesema jaribio la Raila kutwaa wadhifa huo halikuwa la kibinafsi bali la taifa lote la Kenya.

“Tumekuwa katika hali ya wasiwasi wiki moja iliyopita, tukimwombea na kumuunga mkono ndugu yetu Raila Amolo Odinga kuwa Mwenyekiti wa AUC. Ugombea wake haukuwa tu wake, ulikuwa wa Jamhuri ya Kenya na watu wake,” amesema Wetang’ula.

Licha ya pigo hilo, Spika huyo amesisitiza kuwa Kenya itaendelea kuunga mkono ajenda ya AU na maadili ya bara la Afrika.

Ametoa wito wa juhudi zaidi kufanywa hili kuiokomboa Afrika kutoka kwa minyororo ya umaskini na ukosefu wa maendeleo.

“Afrika ndilo bara tajiri zaidi duniani ilhali ni nyumbani kwa watu maskini zaidi. Tunatazamia siku ambapo utajiri mkubwa ilio nao bara letu utaakisiwa katika ustawi wa watu wake.”

Wetang’ula ametoa wito kwa Mwenyekiti mpya wa AUC kufanya kazi na mataifa yote ya Afrika bila kujali yalivyopiga kura zao.

Share This Article