Waziri wa Mazingira Dkt. Deborah Barasa ameilimbikizia Kenya sifa sufufu akisema nchi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira.
Amesema hatua hiyo inawiana na dhamira ya Mkutano wa Ngazi ya Mawaziri wa Afrika Juu ya Mazingira (AMCEN).
“Kenya imefikia maono haya ya Afrika kwa kuchukua hatua za kitaifa na imeonyesha uongozi thabiti katika kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutekeleza sheria na mipango muhimu,” alisema Dkt. Barasa wakati akihutubia kikao cha 20 cha AMCEN katika makao makuu ya Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) jijini Nairobi.
“Kuanzia kwa Sheria ya Mabadiliko ya Tabia Nchi hadi Sheria ya Usimamizi Endelevu wa Taka na Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi, Kenya inaangazia suluhu asilia, uchumi mduara, na jitihada za jamii za kuitunza ardhi na kulinda uhaianuwai.”
Waziri Barasa akisema hatua hizi zinaakisi siyo tu maono ya Kenya, lakini dhamira ya pamoja ya utunzaji endelevu na jumuishi wa mazingira.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Katibu Mkuu wa Tume ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa barani Afrika Claver Gatete miongoni mwa wengine.
Kaulimbiu ya mkutano huo ilikuwa “Miongo Minne ya Hatua za Mazingira Afrika: Kuakisi Yaliyopita na Kutafakari Siku Zijazo.
AMCEN imekuwepo kwa kipindi cha miaka 40 iliyopita, ikitoa kipaumbele katika kupigania masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, uhaianuwai, kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa manufaa ya bara la Afrika katika majukwaa ya kimataifa.